LIBYA-MAREKANI-MUSEVENI-AFRIKA

Museveni:Afrika ilishindwa kuisaidia Libya dhidi ya uvamizi wa mataifa ya kigeni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni REUTERS/Tiksa Negeri/File Photo

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ameyalaumu mataifa ya Afrika kwa kushindwa kuilinda nchi ya Libya dhidi ya uvamizi uliofanywa na mataifa ya Marekani na yale ya jumuiya ya Nato mwaka 2011.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na shirika la utangazaji la Uingereza BBC, rais Museveni amesema nchi za Afrika zilitakiwa kutuma wanajeshi wake kwenda kuilinda Libya dhidi ya uvamizi wa nchi za Magharibi, akisema kinachotokea sasa kilichangia pakubwa na nchi za Afrika kushindwa kuwajibika.

Kauli yake anaitoa wakati huu taifa hilo likishuhudia mzozo wa kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Serikali inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa na wanajeshi wa mbabe wa kivita jenerali Khalifa Haftar.

Dunia kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuisadia Libya kupata amani, baada ya mazungumzo ya amani wiki iliyopita jijini Berlin nchini Ujerumani na kabla ya hapo jijini Moscow nchini Urusi.

Wakuu hao wa dunia kutoka Urusi, Uturuki, Ufaransa na nchi jirani, wamekubaliana kuwa suluhu ya mzozo wa Libya, sio ya kijeshi bali ya kisiasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress, ametoa wito kwa mataifa yanayojihusisha na mzozo huu, kuacha kutuma wanajeshi na silaha nchini humo.

Mazungumzo yajayo yanatarajiwa kufanyika hivi karibuni jijini Geneva.