DRC-TSHISEKEDI-SIASA-MWAKA-MMOJA-MADARAKANI

Changamoto zilizomkumba rais Tshisekedi kwa kipindi cha mwaka mmoja

Rais wa DRC  Félix Tshisékédi.
Rais wa DRC Félix Tshisékédi. ISSOUF SANOGO / AFP

Rais Felix Tshisekedi anatimiza mwaka mmoja siku ya Ijumaa, tangu alipoingia madarakani mwaka 2019, katika nchi hiyo ya Afrka ya Kati ambayo kwa mara ya kwanza ilishuhudia makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani.

Matangazo ya kibiashara

Tarehe 24 mwaka 2019, Tshisekedi alikabidhiwa madaraka kutoka kwa mtangulizi wake Joseph Kabila ambaye alikuwa ameongoza nchi hiyo kwa miaka 18 kwa mkono wa chuma.

Tshisekedi alitokea kwenye upinzani baada ya kuungana na Vital Kamehre na kushinda Uchaguzi huo wa kihistoria ambao hata hivyo, mgombea wa muungano wa Lamuka Martin Fayulu, alidai kuibiwa kura, na hajawahi kukubali ushindi wa Tshisekedi.

Kuingia madarakani kwa rais Tshisekedi, kulileta matumaini mapya kwa wananchi wa DRC ambao waliamini ahadi nyingi za rais wao mpya ambaye kauli mbiu yake ilikuwa ni wananchi kwanza.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake kwa sababu ilimchukua miezi tisa kuunda serikali ya pamoja na chama cha rais wa zamani Kabila na kupelekea kuundwa kwa Baraza la Mawaziri 67.

Ndani ya mwaka huu mmoja, kiongozi huyu wa DRC amejikita katika safari za nje ya nchi hiyo hasa katika nchi ya Ubelgiji koloni ya nchi hiyo lakini pia nchini Marekani na Ufaransa, miongoni mwa mataifa kadhaa barani Afrika.

Miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zimemsumbua rais Tshisekedi katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, ni ukosefu wa usalama Mashariki mwa nchi hiyo hasa Wilayani Beni, eneo ambalo limeshuhudia raia wakipoteza maisha, kutokana na uvamizi la waasi wa ADF Nalu.

Mbali na hilo, maambukizi ya ugonjwa wa Ebola pia eneo la Mashariki mwa nchi hilo, limeendelea kumtesa rais Tshisekedi ambapo kwa kipindi hiki kifupi zaidi ya watu 2, 000 wamepoteza maisha na wengine 3,000 kuambukizwa.

Wakosoaji wake, wanasema rais huyo hajafanya vya kutosha kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kawaida hasa za kiuchumi.

“Tangu aingie madarakani bei ya bidhaa imepanda sana. Hakuna pesa, hatujui itakuwaje,” alisema mfanyibiashara jijini Kinshasa.

Hivi karibuni akiwa jijini London, rais Tshisekedi aliwaambia raia wa nchi yake wanaoishi nchini humo kuwa, hatavumulia Mawaziri ambao wanakwenda kinyume na matakwa yake, huku akitishia kulivunja bunge.