DRC-TSHISEKEDI-SIASA

Félix Tshisekedi atimiza mwaka mmoja madarakani

Sherehe ya kutawazwa kwa Rais mpya wa DRC huko Kinshasa, Januari 24, 2019: Rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila (kushoto) akimpongeza mrithi wake Félix Tshisekedi (kulia).
Sherehe ya kutawazwa kwa Rais mpya wa DRC huko Kinshasa, Januari 24, 2019: Rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila (kushoto) akimpongeza mrithi wake Félix Tshisekedi (kulia). REUTERS/Olivia Acland

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Tshisekedi, ametimiza mwaka mmoja tangu kuchukua hatamu ya uongozi wa nchi hiyo, baada ya kuchukuwa mikoba ya mtangulizi wake Joseph Kabila Kabange.

Matangazo ya kibiashara

Rais Felix Tshisekedi anatimiza mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani, huku raia wa nchi hiyo wakikumbuka ahadi nyingi aliahidi chini ya kauli mbiu yake, "raia kwanza". Wakosoaji wake wanasema ameshindwa katika kutekeleza alichoahidi hadi sasa.

Félix Tshisekedi, mtoto wa mpinzani wa kihistoria nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Etienne Tshisekedi alichaguliwa kama rais baada ya uchaguzi uliozua utata mkubwa.

Hii ilikuwa hatua ya kwanza ya mabadiliko kwa kupishana kwenye madaraka kwa njia ya amani, japokuwa rais Tshisekedi hana nguvu zozote zile za kudhibiti Bunge la kitaifa, na yake mikoa, yanayodhibitiwa na mtangulizi wake Joseph Kabila.

Rais mpya na mtangulizi wake waliamua kuunda muungano badala ya kudumisha mshikamano baina ya wananchi wa DRC.

Hata hivyo kwa sasa kuna mvutano kati ya kambi ya Félix Tshisekedi na kambi ya mtangulizi wake Joseph Kabila.

Hivi karibuni rais Félix Tshisekedi alitishia kuwafuta kazi Mawaziri wake na hata kulivunja bunge, iwapo washirika wake wa kisiasa ambao wanaegemea katika mrengo wa rais wa zamani Joseph Kabila, wataendelea kumdharau.

Tshisekedi alisema kuna baadhi ya Mawaziri ambao wamekuwa wakimwambia kuwa, wanapata shinikizo, na kusisitiza kuwa, hana nia ya kulivunja bunge lakini, iwapo mzozo utazuka, atalazimika kufanya hivyo.

Matamshi yake yamekuja baada ya majuma kadhaa yaliyopita baadhi ya wanasiasa kuzituhumu nchi za ukanda na baadhi ya wanasiasa wa DRC kutaka kuligawa vipande eneo la mashariki mwa DRC.

Rais Tshisekedi ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, aliingia katika maelewano na chama cha zamani wa rais Kabila cha PPRD, kushirikiana naye katika serikali yake, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018.