BURUNDI

Mahakama Burundi yawahukumu kifungo gerezani wanahabari wanne

Picha ya maktaba ikiwaonesha wanahabari 4 wa Burundi walipokuwa katika mahakama ya Bubanza 30/12/2019
Picha ya maktaba ikiwaonesha wanahabari 4 wa Burundi walipokuwa katika mahakama ya Bubanza 30/12/2019 Tchandrou Nitanga / AFP

Mahakama nchini Burundi hivi leo imewahukumu kifungo cha miezi 18 jela, waandishi wanne wa habari baada ya kuwakuta na hatia ya kuripoti habari iliyowahusu waasi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hukumu ambayo tayari imekashifiwa vikali na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International.

Matangazo ya kibiashara

Wanahabari hao wanne walikuwa wakifanya kazi na chombo cha habari cha Iwacu, moja ya vyombo huru nchini humo na walikamatwa tarehe 22 ya mwezi Octoba mwaka jana na kushtakiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa.

"Moja ya mashuhuda waliohudhuria kesi ya wanahabari hao ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, wameshangazwa na hukumu ya kifungo cha miaka 2 na nusu jela na kuwapiga faini ya Franga za Burundi milioni 1."

"Ni aibu kwa sababu wanahabari hao walikuwa wakifanya kazi yao," amesema shuhuda huyo.

Awali waendesha mashtaka wa Serikali walikuwa wameiomba mahakama iwahukumu kifungo cha miaka 15 jela, huku wakitegemea ushahidi wa mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambao ulikuwa ulionesha mawasiliano baina ya wanahabari hao na mmoja aliyeko nje ya nchi, ujumbe ambao ulisema "tunaelekea Bubaza...kuwasaidia waasi."

Muanzilishi wa gazeti la Iwacu, Antoine Kaburahe ambaye anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji, ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kuwa gazeti hilo litakata rufaa.

Polisi nchini humo walisema waasi 14 kutoka kundi la waasi wa Burundi la RED-Tabara waliuawa siku ambayo waandishi hao wa habari nao walitiwa nguvuni.

Kwa upande wao waasi hao ambao wanafanya shughuli zao nchini DRC, wamedai waliwaua wanajeshi kadhaa wa Serikali.

Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International ukanda wa Afrika Mashariki, Seif Magango, amesema hukumu dhidi ya waandishi wa habari, Agnes Ndirubusa, Christine Kamikazi, Egide Harerimana na Terence Mpozenzi imeweka alama mbaya kwa uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari nchin Burundi.

Magango amesema "Mamlaka ni lazima zifute kesi na kubatilisha hukumu dhidi ya waandishi hao wa habari ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru mara moja bila masharti."

Amnesty International inasema wakati huu nchi ya Burundi ikielekea kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu, waandishi wa habari wanapaswa kuachwa kufanya kazi kwa uhuru.

Shirika la wanahabari wasio na mipaka, RSF ambalo limeiorodhesha nchi ya Burundi katika nafasi ya 159 kwenye ripoti yake kuhusu uhuru wa habari duniani, limesema wanahabari waliokuwa wakizuiliwa walikuwa wakitekeleza majukumu yao.