AFRIKA-AU-USALAMA-AMANI

Ramaphosa achukua mikoba ya Abdel Fattah al sisi kama rais wa Umoja wa Afrika

Makao makuu ya Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia.
Makao makuu ya Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia. RFI/Paulina Zidi

Cyril Ramaphosa rais wa Afrika Kusini amekabidhiwa kijiti cha uongozi wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka kwa rais wa Misri Abdel Fattah al sisi, katika mkutano wa Umoja huo huko Addis Abeba nchini Ethiopia.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza mbele ya viongozi wa Umoja wa Afrika, mawaziri, wanadiplomasia, rais wa Misri Abdel Fattah al sisi amesema ilikuwa ni fahari kubwa kwake kuwa kiongozi wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja. Amesisitiza kwamba yupo tayari kuandaa mkutano wa kilele wa kusaidia kuunda jeshi la Afrika kwa ajili ya kupambana na ugaidi, na kisha akamkabidhi kijiti rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Wakati wa hotuba yake, Cyril Ramaphosa amesisitiza juu ya utekelezaji wa Zlecaf, eneo la biashara huria la bara la Afrika, huku akitangaza kufanyika mkutano wa kilele wa Umoja huo Mei 2020 jijini Pretoria.

Cyril Ramaphosa amethibitisha pia kwamba ataitisha mkutano usiokuwa wa kawaida wa wakuu viongozi wa Umoja huo jijini Pretoria mwezi huo huo wa Mei kuzungumzia maswala ya usalama, mkutano ambao kauli mbiu yake itakuwa ni kukomesha mapigano.

Wazungumzaji wote katika kukao hicho wamegusia pia swala la Palestina na kubaini uungwaji wao mkono kwa madai ya Wapalestina. Katika hatua nyingine Cyril Ramaphosa pia alisema kwamba anaunga mkono haki ya kujitawala kwa watu wa Sahara Magharibi, hata akizungumza juu ya serikali huru.

Viongozi wakubwa wa Umoja huo ambao hawakushiriki mkutano huo ni pamoja na rais wa Togo Faure Gnassingbe, ambae yupo katika kampeni za uchaguzi, rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba, ambaye hajaanza kufanya safari za kimataifa tangu pale aliponusurika baada ya kupata kiharusi, rais wa Benin Patrice Talon, , rais wa Cameroon Paul Biya pamoja na mfalme wa Morocco.