MALI-USALAMA

Jeshi la Mali larudi Kidal baada ya kutimuliwa na waasi miaka sita iliyopita

Mnamo mwaka 2014, wanajeshi wa Mali walitimuliwa Kidal, baada ya Waziri Mkuu wa zamani wa Mali Mousa Mara kufanya ziara ya kutatanisha katika mkoa huo.
Mnamo mwaka 2014, wanajeshi wa Mali walitimuliwa Kidal, baada ya Waziri Mkuu wa zamani wa Mali Mousa Mara kufanya ziara ya kutatanisha katika mkoa huo. Wikimédia

Jeshi la Mali limerudi Kidal baada ya kutimuliwa na waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo kutoka jamii ya Tuareg miaka sita iliyopita. Kikosi cha askari 240 walioondoka katika mji wa Bamakao mapema Jumatatu wiki hii na kuwasili katika mji wa kaskazini wa Mali, jeshi limesema.

Matangazo ya kibiashara

Kurudi kwa jeshi la Mali katika Mkoa wa Kidali ni ishara ya ushindi kwa serikali ya Mali, ambayo inajitahidi kurejesha mamlaka yake katika eneo la Kaskazini, na hatua ya kutia moyo katika utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya serikali ya Bamako na waasi wa Tuareg mnamo mwaka 2015. Makubaliano ambayo yanatoa uhuru mkubwa wa kujitawala kwa jamii ya Tuaregs baada ya vikosi vya Mali (FAMA) kurudi katika mkoa huo wa Kidal.

Picha zilizotolewa na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, zinaonyesha Mkuu wa Mkoa wa KIdal, Sidi Mohamed Ag Ichrach, akikaribisha vikosi vya Mali katika mkoa huo unaoshikiliwa na waasi.

Kikosi hiki kinaundwa na theluthi moja ya wanajeshi wa vyeo vya chini, theluthi moja ya waasi wa zamani, na theluthi moja ya wanamgambo wanaounga mkono serikali kuu.

Msafara wa magari ya jeshi la Mali uliambatana na walinda amani na helikopta za tume ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA.

Jumla ya wanajeshi 428 wanatarajiwa kupelekwa katika mkoa wa Kidal katika siku chache zijazo, maafisa wamesema, huku wakibaini kwamba askari wa Mali wataongezwa pole pole hadi maeneo mengine ya Kaskazini mwa nchi.