LIBYA-UN-USALAMA

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé ajiuzulu

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé ametangaza kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba amejiuzulu kwenye nafasi yake. Amebaini kwamba amechukuwa uamuzi huo kwa "sababu za kiafya" baada ya kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili na nusu.

Ghassan Salamé, Desemba 18, 2018, huko Tunis.
Ghassan Salamé, Desemba 18, 2018, huko Tunis. FETHI BELAID / AFP
Matangazo ya kibiashara

"Inanibidi nikiri kwamba afya yangu haniruhusu tena kuendelea kupata mfadhaiko, kwa hivyo nimemuomba katibu Mkuu (wa Umoja wa Mataifa) kunruhusu kuachia ngazi," ameandika Ghassan Salamé, Mfaransa mwenye asili ya Lebanon.

Kujiuzulu kwake kunakuja baada ya mkutano na waandishi wa habari alioendesha Jumamosi Februari 29 huko Geneva baada ya kushindwa kwa mazungumzo ya kisiasa katika ya wadau katika mgogoro unaoendelea nchini Libya.

Katika mkutano huu na waandishi wa habari, Ghassan Salamé alionekana akiwa na ghadhabu dhidi ya kambi zinazohasimiana nchini humo, ambazo haziheshimu ahadi zao walizoafikia huko Berlin, amesema Ghassan Salamé.

Ameshutumu pande zote mbili kwa kueneza uwongo juu ya mazungumzo ya Geneva kuhusu uteuzi wa wawakilishi wanaotakiwa kushiriki kwenye mazungumzo hayo.

"Kwa karibu miaka mitatu, nilijaribu kuwaunganisha Walibya, kuzuia uingiliaji wa mataifa ya nje katika masuala ya n dani ya Libya na kulinda umoja wa nchi," ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.