UFARANSA-BURKINA FASO-COMPAORE-HAKI

Ufaransa yaruhusu François Compaoré kupelekwa Burkina Faso

Serikali ya Ufaransa imeruhusu François Compaoré kupelekwa nchini Burkina Faso kujibu mashitaka yanayomkabili. François Compaoré kaka wa rais wa zamani aliyetimuliwa madarakani nchini Burkina Faso Blaise Compaore anahusishwa katika mauaji ya mwandishi wa habari mwaka 1998.

François Compaoré, kaka wa rais wa zamani wa Burkina Faso, Blaise Compaoré (picha ya kumbukumbu).
François Compaoré, kaka wa rais wa zamani wa Burkina Faso, Blaise Compaoré (picha ya kumbukumbu). Ahmed OUOBA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Sheria ya Burkina Faso imechapisha nakala ya sheria ya kiwaziri, ililosainiwa na Anne Guédamour, msaidizi wa Waziri wa Sheria, Nicole Belloubet.

Akihojiwa na RFI, mwanasheria wa François Compaoré, wakili François Henri Briard, amethibitisha taarifa hiyo, ingawa kwa wakati huu, mteja wake bado hajaarifiwa kuhusu kupelekwa nchini Burkina Faso. Walakini, wakili tayari amepanga kukabiliana na sheria hiyo ya kiwaziri mbele ya baraza la mawaziri. Utaratibu huu kwa kawaida hauizui uamuzi wa serikali kutekelezwa, lakini unasaidia tu kwa upande wa mshataki kucheleweshwa kwa uamuzi huo hadi rufaa zote zitakuwa zimekamilika.

Hata hivyo mawakili wa François Compaoré wamebaini kwamba wako tayari kuwasilisha malalamiko yao mbele ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu huko Strasbourg ikiwa watashindwa. Utaratibu ambao unaweza kuchukua karibu mwaka mmoja.