EU-MAREKANI-CORONA-AFYA

Coronavirus: Umoja wa Ulaya walaani uamuzi wa Donald Trump

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, wakati wa mkutano kwa simu na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Machi 10, 2020.
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, wakati wa mkutano kwa simu na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Machi 10, 2020. Stephanie Leqocq/Pool via REUTERS

Umoja wa Ulaya umesema unasikitishwa na uamuzi wa Marekani ambao umoja huo unasema umechukuliwa na upande mmoja bila hata hivyo kuwasiliana na viongozi wengine duniani kuhusu mripuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani alitangaza kuzuia safari zote za ndege kutoka Ulaya kuingia nchini Marekani kwa siku thelathini Hata hivyo Uingereza na Irland hazilenwi na hatua hiyo. Hatua ambayo imewakera viongozi wa Ulaya.

Rais wa Baraza la Ulaya na Rais wa Tume hiyo, Charles Michel na Ursula von der Leyen wamesema kuwa Marekani imechukua hatua isiyoeleweka na kubaini kwamba mripuko wa ugonjwa wa Covid-19 ni ni janga linalosumbua ulimwengu kwa ujumla, na dunia haitakiwi kutengana kutokana na ugonjwa huo bali ushirikiano ndio jambo muhimu kwa sasa wala sio hatua zinazochukuliwa na upande mmoja.

Umoja wa Ulaya unasema hatua ya Marekani inashangaza na pia inasikitisha. Umoja huo pia umesikitishwa na njia ambayo Marekani ilitumia kwa kuchukua hatua hiyo wakati kuna njia nyingi za kidiplomasia ambazo ingeweza kutumia kwa kutoa taarifa hiyo.

Hata hivyo Umoja wa Ulaya unasema wanajiandaa kujibu hatua hiyo ya Marekani.