TANZANIA-CORONA

Tanzania yathibitisha kisa cha kwanza cha Corona, raia watakiwa kuchukua tahadhari

Waziri wa afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari hawako pichani kuwapa taarifa za uwepo wa mgonjwa wa Corona Tanzania, 16/03/2020
Waziri wa afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari hawako pichani kuwapa taarifa za uwepo wa mgonjwa wa Corona Tanzania, 16/03/2020 Picha kwa Hisani ya Michuzi blogg

Nchi ya Tanzania imekuwa ni taifa jingine kwenye ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kutangaza kisa cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

 

Tangazo la Tanzania linafuatia yale yaliyotolewa na Serikali ya Rwanda ambayo mpaka sasa imethibitisha visa vinne, huku nchi ya Kenya ikithibitisha visa vitatu vya wagonjwa wa Corona mpaka sasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, waziri wa afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, amesema mgonjwa aliyegundulika ni mwanamke raia wa Tanzania aliyewasili Machi 15 kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.

Waziri Ummy amesema mgonjwa huyo aliwasili na ndege ya shirika la Rwanda akitokea nchini Ubelgiji, moja ya taifa ambalo na lenyewe limeathirika pakubwa na virusi hivyo.

“Mgonjwa huyu baada ya kuwasili na kupimwa na wataalamu wetu, hakuonesha dalili zozote, lakini baada ya kufika hotelini anasema alianza kujisikia vibaya ambapo alijitenga kabla ya kwenda hospitalini ambapo baada ya vipimo kuchukuliwa kupelekwa Dar es Salaam, ilithibitika kuwa ana maambukizi ya Corona”. Alisema waziri Ummy.

Kiongozi huyo amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa huo, akiwaelekeza kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuzitaka ofisi na maduka kuweka dawa za vimiminika ambazo wananchi watakuwa wanazitumia kwaajili ya kujikinga.

Katika hatua nyingine, rais w anchi hiyo John Pombe Magufuli, ametangaza kusitishwa kwa mbio maarufu za mwenge wa uhuru, ambapo ameagiza fedha zote zilizokuwa zimepangwa kutumika, zielekezwe katika vita dhidi ya Corona.

Tangazo la Tanzania limekuja wakati huu mataifa karibu 28 ya Afrika yakitangaza hatua kali ikiwemo kuzuia kuingia kwenye mataifa yao, raia wanaotoka nchi ambazo zimeathiriwa na virusi vya Corona.

Siku ya Jumapili nchi ya Kenya ilitangaza kufungwa kwas hule na kuzuia mikutano ya hadhara, sawa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Rwanda na Afrika Kusini.