MALAWI-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi mpya wa urais kufanyika Julai 2 nchini Malawi

Tume ya Uchaguzi nchini Malawi (MEC) imetangaza kwamba uchaguzi mpya wa urais nchini humo utafanyika Jumatatu, Julai 2, 2020 baada ya Mahakama kufuta uchaguzi wa Mei 2019 uliyompa ushindi rais anayemaliza muda wake Peter Mutharika.

Wananchi wa Malawi wapiga kura Mei 21 2019
Wananchi wa Malawi wapiga kura Mei 21 2019 MBC
Matangazo ya kibiashara

Mahakama ya Katiba ilichukuwa uamuzi wa kufutilia mbali uchaguzi huo kutokana na dosari nyingi zilizoufanya uchaguzi huo usiwe huru, haki na wa kuaminika, alisema Jaji kiongozi wa Mahakama ya Katiba, Healey Potani.

Mahakama ya Katiba ya Malawi iliitaka Tume ya uchaguzi (MEC) kusitisha kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Mei 21 kwa sababu ya madai ya udanganyifu.
Mahakama ya Katiba ya Malawi iliitaka Tume ya uchaguzi (MEC) kusitisha kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Mei 21 kwa sababu ya madai ya udanganyifu. AMOS GUMULIRA / AFP

"MEC inatangaza kwamba uchaguzi wa urais utafanyika Julai 2," Mwenyekiti wa tume hiyo, Jane Ansah, amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Mei 21 mwaka 2019, Tume ya uchaguzi ilimtangaza Peter Mutharika kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 38.6 ya kura zote.

Matokeo hayo kwa majuma kadhaa yalisababisha maandamano makubwa ya wafuasi wa upinzani, huku serikali ikilaumiwa pakubwa kwa kutumia nguvu kubwa kukabiliana na waandamanaji.

Tume ya haki za binadamu nchini Malawi imesema mwezi Oktoba pekee wakati wa maandamano ya wafuasi wa upinzani, polisi na wanajeshi walitekeleza vitendo vya ukatili kwa kuwabaka wanawake hata mbele ya familia zao.