Ituri: FARDC yadhibiti kijiji cha Kpandroma kutoka mikononi mwa wanamgambo wa CODECO
Imechapishwa:
Watu kadhaa wameuawa baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa kundi la CODECO katika Mkoa wa Ituri, mauji ambayo yamekuja baada ya jeshi kutangaza kuuawa kwa kiongozi wa kundi hilo.
Mwishoni mwa wiki hii, vikosi vya ulinzi (FARDC) vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) vilidai kuwa vilidhibiti kijiji cha Kpandroma bila mapigano yoyote Jumamosi Machi 28.
Kpandroma ni kijiji ambacho kinapatikana kilomita 140 Kaskazini Mashariki mwa Bunia katika Wilaya ya Djugu (Ituri).
Kwa mujibu wa kaimu mkuu wa jeshi la DRC, katika Jimbo la Ituri, Jenerali Yav Aul Ngol Robert, kijiji cha Kpandroma kilikuwa mikononi mwa wanamgambo wa CODECO kwa wiki kadhaa.
Amesema lengo la jeshi ni kurejesha mamlaka ya serikali katika eneo hilo. Huko Kpandroma, wanamgambo wa kundi la CODECO walikuwa na mamlaka kamili, ikiwa ni pamoja na kutoza ushuru na kuweka mahakama za kijadi.
Jenerali Yav Aul Ngol Robert amewatolea wito wanamgambo wa kundi hilo kujisalimisha haraka iwezekanavyo, huku akionya kwamba vikosi vya jeshi vitaendelea kudhibiti vijiji na maeneo yote ambayo yanashikiliwa na adui katika Wilaya ya Wencu Pisti.
Wakazi wengine ambao walikuwa wametoroka makazi yao katikati kijiji cha Kpandroma kwa kuhofia usalama wao kufuatia mapigano kati ya askari na wanamgambo wa CODECO wameanza kurudi tangu Jumapili Machi 29 asubuhi, kwa mujibu wa Radio Okapi, ambayo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO.