IGAD-CORONA-AFYA

Coronavirus: Nchi wanachama wa Igad kuunda mfuko wa kuzuia maambukizi

Wajumbe wa Igad, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki, wawamekutana Jumatatu wiki hii kwa mkutano wa dharura kuhusu janga la Covid-19. Mkutano ambao ulifanyika kupitia video.

Maafisa wa afya wakipulizia dawa dhidi ya virusi vya Corona huko Nairobi, Kenya, Machi 2020.
Maafisa wa afya wakipulizia dawa dhidi ya virusi vya Corona huko Nairobi, Kenya, Machi 2020. REUTERS/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Kadiri ugonjwa huo unavyoenea pole pole katika bara la Afrika, nchi hizo saba za Afrika Mashariki na ukanda wa Pembe la Afrika zina wasiwasi mkubwa.

Rais wa sasa wa Igad, Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok, alifungua mijadala ya mkutano huo wa kipekee kupitia video. Mataifa hayo saba wameweka kando tofauti zao ili kukabiliana na ugonjwa huo hatari duniani. "Ulimwengu haukujiandaa. Leo ushirikiano ni muhimu, "Rais wa Somalia Mohamed Farmajo alisema.

Igad imeamua kufungua mfuko wa kudhibiti na kuzuia kuenea kwa virusi vinavyo sababisha ugonjwa wa Covid-19. Rais wa Djibouti Ismaël Omar Guelleh, amesema utakuwa "udhamini wa thamani wa kuimarisha mifumo ya tahadhari, uangalizi na matarajio". Kiasi cha fedha bado hakijajulikana, lakini wakati wa mkutano uliyopita wa nchi zinazostawi kiuchumi na kiviwanda, G20, Waziri Mkuu wa Ethiopia alikadiria dola bilioni 150, kama mahitaji ya Afrika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Ulaya tayari kwa msaada

Igad pia inaomba jamii ya kimataifa kupunguza mzigo wa madeni na kuwarahisishia kupata mikopo. Inatafuta pia msaada wa kujenga miundombinu katika ukanda huo na kupunguza kuingiza vifaa vya matibabu katika nchi wanachama. Kenya tayari imepanga kuzindua zoezi la kutengeneza maski na barakoa kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Mawaziri wa fedha wa nchi za ukanda huo na wale wa afya watakutana hivi karibuni kutathmini mahitaji hayo. Tume ya Umoja wa Ulaya tayari imejibu wito huo, ikitangaza kuwa tayari kutoa msaada. Kenya, kwa mfano, ambayo ina visa 50 vya maambukizi ya virusi vya Corona, ina hofu ya kupatikana maambukizi mapya 5,000 ndani ya wiki mbili.