NIGER-SIASA-HAKI

Kiongozi wa upinzani Niger aachiliwa huru kwa msamaha wa rais

Kiongozi wa upinzani nchini Niger, Hama Amadou, ameondolewa katika jela la Filingué ambapo alikuwa akizuiliwa kwa tuhuma ya biashara ya watoto.
Kiongozi wa upinzani nchini Niger, Hama Amadou, ameondolewa katika jela la Filingué ambapo alikuwa akizuiliwa kwa tuhuma ya biashara ya watoto. BOUREIMA HAMA / AFP

Hatimaye Kinara wa upinzani nchini Niger Hama Amadou ameachiliwa huru pamoja na wafungwa wengine zaidi ya elfu moja, kutokana na msamaha wa rais ambaye ameamua kupunguza wafungwa Magerezani kama hatua ya kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyu wa upinzani nchini Niger Hama Amadou ameondolewa katika jela la Filingué hapo jana ambapo alikuwa akizuiliwa kwa tuhuma ya biashara ya watoto.

Hama Amadou ameachiliwa huru pamoja na wafungwa elfu moja mia tano arobaini kufwatia msamaha wa rais Mahamadou Issoufou ambaye alitangaza kuwa lengo hasa ni kupunguza idadi ya wafungwa kwenye magereza, wakati huu nchi yake ikipambana na maambukizi zaidi ya virusi vya Corona.

Tangazo la kuachiliwa huru kwa kinara huyo wa upinzani nchini Niger lilipokelewa kwa furaha kubwa na wafuasi wake katika mji wa Niamey hapo jana, na kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wanaharakati wa upinzani na hasa wale wa chama chake, Moden Fa Lumana, wakimpongeza rais wa nchi hiyo.

Hama Hamadou alikuwa akiishi uhamishoni nchini Ufaransa, alirudi nchini Niger kwa hiari yake miaka minne iliyopita kutumikia kifungo kilichokuwa kimebaki katika kesi dhidi yake ya kusafirisha watoto nchini Nigeria.