LIBERIA-CORONA-AFYA

Liberia yaagiza raia wake kubaki nyumbani

Moja ya maeneo yanayotembelewa na watu wengi jijini Monrovia, Liberia.
Moja ya maeneo yanayotembelewa na watu wengi jijini Monrovia, Liberia. Darlington Porkpa

Rais wa Liberia George Weah ametangaza hali ya dharura nchini kote raia kutoka mikoa kadhaa, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Monrovia, wakitakiwa kubaki nyumbani, katika kupambana na kuenea kwa Ugonjwa wa Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Nyota wa zamani wa mpira wa miguu, ambaye yuko madarakani tangu mwezi Januari 2018, ametangaza runinga kwamba ni marufuku kusafiri kati ya kaunti 15 za nchi hiyo maskini Afrika Magharibi. Hatua ambayo itaanza kutekelezwa Ijumaa saa 11.59 usiku.

Makampuni yote na kazi za serikali zisizo muhimu zitafungwa.

Wakazi wa kaunti nne, ikiwa ni pamoja na Monrovia (yenye wakazi karibu milioni moja), watalazimika kukabaki nyumbani kwa wiki mbili, rais wa Liberia ameongeza.

Katika kipindi hiki, mtu mmoja tu kwa kila familia ataruhusiwa kutoka, karibu na eneo la makazi yake, kununua chakula au kwa sababu za matibabu, na kwa muda usio zidi saa moja.

"Lazima tujiulize kwa nini tunapaswa kuheshimu hatua hizi. Jibu ni rahisi: kuokoa maisha ya watu," mshambuliaji nyota wa PSG na AC Milan katika miaka ya 1990 amebaini.

Hatua hizi mpya zinakuja kuongezea nguvu hatua zingine ambazo zilichukuliwa hivi karibuni, kama vile marufuku ya mikusanyiko na kuzifungia ndege kutoka nchi zilizoathiriwa na Covid-19 kuingia nchini Liberia.

Kama ilivyo katika nchi zingine za Kiafrika, wataalam wana hofu kwamba mfumo wa afya hautaweza kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo kwa wakazi karibu milioni 4.8, ambao wengi wao wanaishi katika hali ya umaskini.

Nchi hiyo, ambayo inaendelea kuimarisha uhusiano wa karibu na Marekani, imetangaza visa 13 vya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 na vifo vitatu.

Hata hivyo, George Weah amebaini kwamba Liberia inakabiliwa na tishio kubwa zaidi tangu kuzuka kwa janga la Ebola lililoua zaidi ya watu 4,800 kati ya mwaka wa 2014 na 2016.