Mahakama ya Haki ya Afrika yasitisha waranti dhidi ya Guillaume Soro
Imechapishwa:
Mahakama ya Haki ya Afrika imesitisha waranti dhidi ya Guillaume Soro. Uamuzi ambao ulitolewa Jumatano wiki hii. Mahakama hiyo ya Umoja wa Afrika pia imeomba kuachiliwa kwa ndugu zake 19 ambao wanazuiliwa tangu miezi 4 iliyopita.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, taasisi ya Umoja wa Afrika yenye makao yake makuu jijini Arusha, nchini Tanzania, ambayo Guillaume Soro na ndugu zake waliitaka iingile kati, "inaiagiza serikali ya Cote d'Ivoire kusitisha utekelezaji wa waranti wa kukamatwa dhidi ya Guillaume Soro", katika uamuzi uliotolewa Jumatano wiki hii.
Guillaume Soro, aliyejitangaza kwamba atawania katika uchaguzi wa urais nchini Coted'Ivoire uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Guillaume Soro anakabiliwa na waranti wa kukamatwa uliotolewa tangu mwishoni mwa mwezi wa Desemba 2019 na mahakama ya Cote d'Ivoire akishtumiwa kuanzisha "uasi", na ubadhirifu wa mali ya umma, mashtaka yalikanushwa na kiongozi huyo wa zamani wa waasi katika miaka ya 2000.