COTE D'IVOIRE-SORO-SIASA-USALAMA

Waziri mkuu wa zamani wa Cote d'Ivoire ahukumiwa kifungo cha miaka 20

Guillaume Soro huko Paris, Januari 29, 2020.
Guillaume Soro huko Paris, Januari 29, 2020. Lionel BONAVENTURE / AFP

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Cote d'Ivoire na kiongozi wa zamani wa waasi Guillaume Soro amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana  na kosa la wizi na utakatishaji wa fedha.

Matangazo ya kibiashara

Guillaume Soro ambaye yuko ukimbizini nchini Ufaransa, hakuwepo wakati hukumu hiyo ilipotolewa na mahakama ya Abidjan Jumanne wiki hii.

Guillaume Soro na wanasheria wake wanasema hukumu hiyo ilitolewa na mahakama baada ya kushinikizwa ili kumzuia kuwania nyadhifa ya uongozi nchini humo.

Hivi karibuni Guillaume Soro alitangaza kuwania katika uchaguzi wa urais ujao nchini humo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Soro anashtumiwa kwamba alitumia fedha za umma takriban Euro Milioni Saba kujinunulia makaazi ya kifahari jijni Abidjan mwaka 2007 alipokuwa waziri mkuu.

Hata hivyo washirika wake wa karibu ikiwa ni pamoja na ndugu zake, wabunge na wafuasi wake wanaendelea kuzuiliwa nchini Cote d'Ivoireb baada ya kukamatwa tangu mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana.

Kulingana na wanasheria wao, kesi hii ni ya kisiasa na ilianza kwa sababu Guillaume Soro, mshirika wa zamani wa Alassane Ouattara, aliachana naye na kutangaza kuwania katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.