KENYA-SOMALIA-AJALI-USALAMA

Ndege ya mizigo kutoka Kenya yaanguka Somalia, sita wafariki dunia

Somalia imeendelea kukumbwa na visa vya mashambulizi ya hapa na pale.
Somalia imeendelea kukumbwa na visa vya mashambulizi ya hapa na pale. REUTERS/Feisal Omar/File Photo

Watu sita wamepoteza maisha katika ajali ya ndege ya mizigo iliyoanguka Jumatatu nchini Somalia, wakati ilikuwa ikisheheni msaada, wizara ya mambo ya nje ya Kenya imesema Jumanne wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na gazeti la kila siku la Daily Nation, ndege hiyo ilidunguliwa na viongozi wa Kenya wameomba Somalia kufanya uchunguzi kuhusu "mazingira ya tukio hilo" ambalo "halieleweki".

Ndege hiyo ya kibinafsi ya mizigo kutoka Kenya- Embraer 120 - ilikuwa imesheheni vifaa kama sehemu ya mapambano dhidi ya janga la Corona wakati ilipoanguka Jumatatu alasiri katika wilaya ya Bardale Kusini mwa Somalia, wizara ya mambo ya nje ya Kenya imebaini.

Watu sita walio katika ndege hiyo iliyokuwa ikifanya safari fupi kutoka Baidoa kwenda Bardale, kilomita 300 Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, walipoteza maisha, mamlaka imesema.

"Ndege ilikuwa karibu kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bardale wakati ilianguka na kuwaka moto. Watu sita waliokuwemo katika ndege hiyo walifariki dunia katika ajali hiyo," afisa wa polisi katika eneo hlilo Abdulahi Isack ameliambia kwa simu shirika la habari la AFP.

Kundi la Al-Shabab lina ngome zake Kusini mwa Somalia, lakini eneo ambalo ajali hiyo ilitokea huko Bardale liko chini ya himaya ya serikali na kikosi cha jeshi la Umoja wa Afrika kutoka Ethiopia lililotumwa kusimamia amani nchini Somalia.

Meja Jenerali Mohammed Tessema, msemaji wa jeshi la ulinzi la kitaifa la Ethiopia, amesema hana taarifa kuhusu ajali hiyo.

Wizara ya Uchukuzi na Anga ya Somalia imesema katika taarifa kwamba "inahuzunishwa atukio hilo" na kwamba serikali itafanya "uchunguzi wa kina".

Wizara hiyo imeongeza kuwa ndege hiyo iilikuwa ikitumiwa na shirika la African Express, lenye makao yake makuu jijini Nairobi.

Kulingana na Daily Nation, marubani wote wawili walikuwa ni raia wa Kenya na watu wengine wanne walikuwa raia wa Somalia.