AFRIKA KUSINI-CORONA-UCHUMI

Raia wa Afrika Kusini wakaribisha hatua ya kulegeza masharti ya kubaki nyumbani

Kiwanda cha makaa ya mawe katika mkoa wa Mpumlanga, Afrika Kusini (picha ya kumbukumbu).
Kiwanda cha makaa ya mawe katika mkoa wa Mpumlanga, Afrika Kusini (picha ya kumbukumbu). REUTERS/Siphiwe Sibeko

Shughuli za kawaida zimeanza kurejea tena tangu Jumatatu wiki hii nchini Afrika Kusini, huku raia wa nchi hiyo wakipongeza hatua ya kulegeza masharti ya kubaki nyumbani iliyokuwa imewekwa kwa kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Hali hiyo inakuja baada ya rais Cyril Ramaphosa mwezi uliopita kutangaza kuwa shughuli za kiuchumi, zitaanza kurejea popole wiki hii katika taifa hilo ambalo limeshuhudia watu zaidi ya 6,000, wakiambukizwa  virusi vya Corona.

Milolongo mirefu ya watu imeendelea kushuhudiwa katika vituo vya magari katika miji mbalimbali nchini Afrka Kusini ikiwa ni juhudi ya serikali kulegeza marufuku ya watu kutotembea baada ya mlipuko wa virusi vya Corona.

Wengi walionekana wakiwa wamevalia barakoa baada ya wito wa serikali huku wengine wakionekana na vitakaza mikono na kukaa  mbali na wengine.

Magari ya uchukuzi wa umma yametakiwa kubeba abiria wachache  kama njia mojawapo ya kuendelea kupambana na janga hili ambalo limesababisha zaidi ya watu 130 kupoteza maisha.

Pamoja na hatua hii, serikali inaendelea kutoa wito kwa wanaoweza kufanya kazi wakiwa nyumbani kufanya hivyo ili kuzuia maambukizi zaidi.