DRC-KAMERHE-HAKI-CORONA-AFYA

Coronavirus DRC: Vital Kamerhe kuachiliwa huru

Vital Kamerhe alisimamia mpango wa dharura kwa siku 100 za kwanza katika serikali ya rais Tshisekedi.
Vital Kamerhe alisimamia mpango wa dharura kwa siku 100 za kwanza katika serikali ya rais Tshisekedi. REUTERS/Baz Ratner

Kutokana na kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini DRC, mamlaka nchini humo wana wasiwasi juu ya hatari ya kuenea kwa virusi hivyo katika jela mbalimbali nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hatua za kuwaachilia huru wafungwa zinatarajiwa kutangazwa nchi kote DRC.

Vital Kamerhe, mkurugenzi wa afisi ya rais Félix Tshisekedi, ambaye anazuiliwa jela kwa mwezi mmoja sasa akisubiri kesi yake, ambayo imepangwa kuanza Mei 11, ni miongoni mwa watu wanaopewa nafasi kubwa ya kunufaika na hatua hizo.

Upande wa utetezi wa Vital Kamerhe una matumaini makubwa kuhusu kuachiliwa kwa mteja wao, baada ya baraza la mawaziri kuzungumzia suala hilo wakati wa kikao chake Jumatatu wiki hii.

Kwa sasa, bado zoezi hilo halijaanza, Wizara ya Sheria na Wizara ya Haki za Binadamu zinatengeneza orodha ya watu ambao watanufaika na hatua hiyo ya kuwaachilia huru kwa muda. Woizara hizi mbili ziko chini ya shinikizo kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kwamba kuna wafungwa wengine wengi ambao kesi zao hazijaanza, kuna hata wafungwa ambao wamemaliza kifungo chao na bado wanasalia jela na wengine ambao walipewa msamaha na rais lakini hawajafunguliwa tangu miaka kadhaa iliyopita.

Hata hivyo kwa mujibu wa vyanzo kutoka ofisi ya Naibu Waziri mkuu mwenye dhamana ya sheria, kipaumbele kinapaswa kutolewa kwa wanawake wajawazito, watoto na watu ambao hali yao ya afya ni dhaifu.