NIGERIA-USALAMA

Watu 60,000 wayatoroka makazi yao Nigeria kufuatia machafuko

Maradi, mji wa tatu kwa ukubwa nchini Niger. Wanigeria wengi wamepewa hifadhi ya ukimbizi katika mji huu tangu mwaka mmoja uliyopita.
Maradi, mji wa tatu kwa ukubwa nchini Niger. Wanigeria wengi wamepewa hifadhi ya ukimbizi katika mji huu tangu mwaka mmoja uliyopita. PIUS UTOMI EKPEI / AFP

Machafuko yanayoendelea kulikumba eneo la Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria yamesababisha takriban watu 23,000 kukimbilia nchini Niger kwa kuhofia usalama wao kwa kipindi cha mwezi wa Aprili 2020 pekee.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi HCR limesema lina wasiwasi na kutokea na mgogoro wa kibinadamu kufuatia machafuko hayo.

Machafuko ya wa hivi karibuni yamesababisha watu wengine wengi kuyatoroka makazi yao na kufanya zaidi ya watu 60,000 kutoroka eneo hilo la Kaskazini-Magharibi mwa nchi tangu kutokea kwa kwa mara ya kwanza tukio kama hilo la watu kuyatoroka makazi yao mnamo mwezi wa Aprili 2019.

Watu wanaotafuta ulinzi wanaruhusiwa kuingia nchini Niger licha ya kufungwa mipaka kwa sababu ya janga la Covid-19.

Kulingana na ushuhuda uliokusanywa na Shirika la Umoja aw Mataifa linalohudumia Wakimbizi, ukosefu wa usalama ndio ulisababisha watu 23,000 kutoroka makazi yao kaskazini-Magharibi mwa Nigeria na kukimbilia nchini Niger mwezi uliyopita.

Wakimbizi hawa ni wanawake na watoto ambao ni kutoka majimbo ya Sokoto, Zamfara na Katsina.

Wakimbizi hawa wanaokimbia wanakumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayoendeshwa na makundi ya wahalifu katika majimbo haya matatu. Mashambulizi ambayo yamedumu sasa miezi kadhaa. Mashahidi wanaripoti unyanyasaji uliokithiri dhidi ya raia, mauaji, utekaji nyara kwa kutarajia fidia na visa vya uporaji katika vijiji mbalimbali.

Wengi wanasema walihofia kushambuliwa na majeshi ya serikali yanapojimbu mashambulizi ya makundi hayo ya wahalifu. Ndege ya jeshi la Nigeria ilitekeleza mashambulizi dhidi ya ngome zinazodaiwa kuwa za makundi hayo ya wahalifu katika jimbo la Katsina mwezi wa Aprili mwaka huu, kwa mujibu wa mashahidi hao.