Burkina Faso: Wafungwa 12 wanaotuhumiwa ugaidi wapatikana wamefariki dunia katika jela
Imechapishwa:
Wafungwa 12 waliokuwa wakizuiliwa katika kituo cha polisi cha Tanwalbougou katika mkoa wa mashariki mwa Burkina Faso wamepatikana wamekufa katika jela hilo. Tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 11 kuamkia Mei 12 walipokuwa kizuizini. Uchunguzi umeanzishwa ili kujuwa sababu za tukio hilo.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, watu ishirini na tano walikamatwa na vikosi vya ulinzi na usalama usiku wa Mei 11 kuamkia Mei 12. Watu hao ambao walikuwa wakishtumiwa ugaidi, walikuwa kizuizini katika kituo cha polisi huko Tanwalbougou, kilomita 40 kutoka mji wa Fada N'Gourma.
Saa chache baadae wafungwa kumi na mbili kati yao walifariki dunia. "Walifariki dunia usiku kwa kukosa hewa walipokuwa wakizuiliwa sehemu moja," kilisema chanzo cha usalama, kabla ya taarifa kutoka kwa mwendesha mashitaka. Chanzo hicho kimeongeza kuwa waliokamatwa walipaswa kuhojiwa kabla ya kupelekwa katika jela kuu.
Uchunguzi umeanzishwa. Maafisa wa polisi tayari wamezuru eneo hilo kwa ukaguzi zaidi wakiandamana na maafisa wa afya, alisema mwendesha mashtaka wa Faso.
Muungano wa mashirika ya kiraia umehoji kuhusu mazingira ambapo watu hao kumi na mbili waliuawa.