DRC-ITURI-USALAMA

DRC: Machafuko yaendelea kuongezeka Ituri

Askari wa FARDC katika kanisa moja huko Djugu, Ituri, inayokumbwa na machafuko (picha ya kumbukumbu).
Askari wa FARDC katika kanisa moja huko Djugu, Ituri, inayokumbwa na machafuko (picha ya kumbukumbu). John WESSELS / AFP

Katika miezi ya hivi karibuni, madhambulio kadhaa yameripotiwa katika maeneo 4 kati ya 5 ambayo yanaunda mkoa wa Ituri, Kaskazini-Mashariki mwa Jamhuri ya KIdemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Wiki hii, Wabunge na Maseneta kutoka Ituri walikutana na Jeanine Mabunda na Alexis Thambwe Mwamba, Rais wa Bunge la Kitaifa na Spika wa Bunge la Seneti, ili kuomba hatua zaidi kutoka kwa mamlaka zichukuliwe dhidi ya makundi yanayohusika na machafuko hayo.

Alhamisi, Mei 14, vijana wa maeneo kadhaa ya mkoa wa Ituri walimiminika mitaani huko Mahagi, huku awkizuia barabara kuu ya eneo hilo. Waliandamana dhidi ya kuongezeka kwa machafuko katika mkoa wao. Mahagi ni moja wapo ya wilaya ambazo zimeathirika pakubwa na shambulio la hivi karibuni la wanamgambo wa Codeco wiki tatu zilizopita.

Pia hali ni ya wasiwasi katika Wilaya ya Walendu Watshi, kwenye mpaka na eneo la Djugu, ambalo kwa muda mrefu lilioneka kuwa ni kitovu cha machafuko.

Katika eneo la Djugu, wanamgambo wa kundi la Codeco wamegawanyika katika makundi madogo madogo na kulazimisha jeshi kubadili mkakati wake wakati wowote.

Wiki iliyopita, mapigano mapyayalitokea huko Bese, katika Wilaya ya Baniali-Kilo, ambapo jeshi la FARDC lilitangaza kuua wanamgambo 17.

Katika eneo la Mambasa, wanamgambo wa Mai-Mai ndio wanaendelea kuhatarisha usalama wa raia. Mara nyingi wanapora na kushambulia migodi ya dhahabu inayomilikiwa na kampuni kutoka China. Mara kwa mara, kwenye mpaka na Mkoa wa Kivu Kaskazini, wapiganaji wa kundi la waasi wa Uganda la ADF pia huendesha mashambulizi.

Katika eneo la Irumu, wanamgambo wa kundi la Shini ya Kilima wakati mwingine wanashambulia ngome za jeshi katika kujaribu kupora silaha na risasi. Huko Kinshasa, vyanzo kutoka ofisi ya rais wa Jamhuri vinatangaza kwamba maafisa wa polisi na askari wanatarajiwa kupelekwa Ituri katika siku zijazo kusaidia wenzao.