Cameroon: Askofu mkuu wa Douala aonyesha 'dawa' yake dhidi ya ugonjwa wa Covid-19
Imechapishwa:
Wizara ya Afya ya Cameroon inasema inaendelea kuwa makini juu ya ubora wa dawa ya mitishamba iliyotengenezwa na Askofu mkuu wa Douala ambayo inadaiwa kuwa inatibu ugonjwa wa Covid-19.
Licha ya kuwa Askofu Kleda ametaa kuweka wazi muundo wa dawa hiyo, amebaini kwamba ameshafanya majaribio kwa wagonjwa kadhaa na baadhi wamepona na nwengine wanaendelea vizuri.
Dawa hii ya mitishamba inatumiwa kwa kunywa baada ya kuichanga na maji safi mara kadhaa kwa siku, amesema Askofu mkuu wa Douala, huku akibaini kwamba huondoa haraka virusi vya Corona kwa mgonjwa anayeitumia.
"Kwa wiki moja inatosha, mgonjwa anakuwa amepona. Lakini maumivu hupotea ndani ya saa ishirini na nne. Kati ya wale wote ambao wametumia dawa hii kufikia sasa - ni watu 900 - hakuna aliyefariki dunia, " amesema Askofu Kleda.
Taarifa hizi za Askofu Mkuu zimezua sitofahamu nchini Cameroon. Lakini hakuna dawa hii haijaungwa mkono na serikali wala wanasayansi nchini Cameroon
Mapema mwezi Mei, timu kutoka Wizara ya Afya ilikwenda Douala kukutana na Askofu Mkuu Kleda na kukubaliana naye "kuandamana" naye "kutathmini nguvu ya dawa hiyo na jinsi invyotumiwa", amesema Dk Vanli, mkurugenzi wa maduka ya dawa kwenye wizara ya afya.
Kwa upande wake Dk Gervais Atedjoe, katibu mkuu wa Chama cha Madaktari nchini Cameroon amejizuia kuzungumzia kuhusu matumizi ya dawa hiyo: "Katika kile kinachojulikana kwa matibabu unapotumia dawa za kisasa, inatakiwa kwanza ili dawa itumiwe lazima iwe imeidhinishwa. Sisemi kwamba dawa hii inafanya kazi, wala sisemi kwamba haifanyi kazi, kwa sababu uthibitisho wowote. "
Hata hivyo Askofu Mkuu wa Doula anasema yuko tayari kutoa dawa yake bila malipo kwa mtu yeyote anayetaka, na amepata uungwaji mkono lakini pia msaada wa kifedha kutoka kwa wafadhili wengi, watu wasiojulikana, wafanyabiashara, au viongozi wa kisiasa wa upinzani, ukianzia kwa Maurice Kamto.
Kufikia sasa hakuna kitu kinachoonyesha ubora wa dawa hiyo dhidi ya Covid-19.
Shirika la Afya Duniani linasema kwamba halipingani na dawa za jadi, lakini linasisitiza juu ya umuhimu wa kuweka kila dawa kwa majaribio ya kliniki, ili kuhakikisha ubora wake.