DRC-KAMERHE-UCHUMI-HAKI

DRC: Waziri wa Elimu ya Ufundi John Ntumba apoteza kinga ya ubunge

Daraja linalojengwa kwenye barabara kuu Mandela huko Kinshasa, moja ya miradi katika "mpango wa siku 100" wa rais Félix Tshisekedi.
Daraja linalojengwa kwenye barabara kuu Mandela huko Kinshasa, moja ya miradi katika "mpango wa siku 100" wa rais Félix Tshisekedi. AFP Photos/Junior Kannah

Bunge la kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limemvua kinga ya ubunge John Ntumba na hivyo kuidhinisha mahakama kuendelea na utaratibu wa sheria dhidi ya Waziri huyo wa Emilu ya Ufundi.

Matangazo ya kibiashara

John Ntumba anashtumiwa kutumia vibaya mali ya umma katika kesi inayohusu mpango wa siku 100 wa rais Felix Tshisekedi.

Taarifa zilizokusanywa na ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma kutoka Mahakama ya Rufaa ya Kinshasa-Matete inaonyesha kwamba John Ntumba, ambaye ni mjumbe wa kamati ya uangalizi ya "mpango wa siku 100", anadaiwa kuwa alipokea kitita cha Dola Milioni 1.3 kutoka kwa José Ngunda Mulumbu, mhasibu mkuu wa ofisi ya rais Julai 18, 2019. Fedha ambazo zimekuwa zimetengwa katika matumizi ya mpango wa siku 100.

Kulingana na mashtaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, fedha hizo haijulikani wapi zilipelekwa. Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka, kitendo hicho kinaweza kuwa kosa la matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kufikia sasa John Ntumba anaweza kutekeleza majukumu yake kama waziri. John Ntumba ni mmoja wa vigogo wa chama UNC, cha Vital Kamerhe, mkurugenzi wa ofisi ya rais Félix Tshisekedi, ambaye pia anashutumiwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika mpango wa dharura wa siku 100.