MALI-HAKI

Mali: Mwanaharakati anayepambana dhidi ya ufisadi Clément Dembélé achiliwa baada ya kukamatwa

Mji mkuu wa Mali, Bamako, Machi 21, 2017.
Mji mkuu wa Mali, Bamako, Machi 21, 2017. SEBASTIEN RIEUSSEC / AFP

Mwanaharakati anayeendesha vita dhidi ya ufisadi nchini Mali Clément Dembélé ameonekana tena Ijumaa Mei 22 baada ya kufikishwa mbele ya mwendesha mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Alikamatwa Mei 9, na kushtakiwa kosa la "kushawishi wanajeshi kwa kukaidi serikali na kuanzisha ghasia", mashtaka ambayo hayana uhusiano kabisa na shughuli zake za kupambana na rushwa.

Baada ya kuachiliwa huru, ametakiwa kuripo tena mahakamani Julai 1.

Baada ya kukaa kizuizini kwa muda wa siku 13, Clément Dembélé alizungumza na waandishi wa habari kwa lugha ya taifa nchini Mali. Alikamatwa na idara ya ujasusi nchini Mali, kabla ya kukabidhiwa vyombo vya sheria nchini humo. Alisikilizwa na mwendesha mashtaka Ijumaa Mei 22.

"Ninashutumiwa kutoa wito kwa wanajeshi kukaidi serikali," Clement Dembélé amesema mbele ya umati wa watu ambao walikuja kumsikiliza. Nina imani na vyombo vya sheria nchini Mali, "ameongeza mwanaharakati huyo anayeendesha vita dhidi ya ufisadi kabla ya kuwashukuru wale wote waliomuunga mkono wakati alipokuwa kizuizini.