Coronavirus: Afrika Kusini yajiandaa kulegeza masharti mengine, maambukizi zaidi yathibitishwa
Imechapishwa:
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema maambukizi ya virusi vya Corona nchini mwake vinaendelea kuongezeka kama ilivyobashiriwa na wanasayansi.
Katikati mwa wiki iliyopita wanasayansi nchini Afrika Kusini walionya kuwa huenda watu 50,000 wakapoteza maisha na wengine zaidi ya Milioni tatu, kuambukizwa virusi vya Corona kufikia mwisho wa mwaka huu.
Wizara ya afya nchini humo iliwaajiri Wanasayansi hao kutoa taswira ya maambukizi hayo, na kubainika kuwa huenda kati ya watu 35,000 na 50,000 wakapoteza maisha kufikia mwezi Novemba.
Licha ya ongezeko hilo, kiongozi huyo amesema kuwa ifikapo tarehe 1 mwezi Juni, serikali itandoa masharti mengine ili maisha yaendelee kama kawaida.
Afrika Kusini kwa sasa ina visa vya maambukizi 22,583 baada ya visa vipya 1,240 kuthibitishwa. Wagonjwa 10,104 wamethibitishwa kupona ugonjwa wa Covid-19, ugonjwa ambao kufikia sasa umeua watu 429.
Raia wa nchi hiyo wametakiwa kuanza kuzoea kuishi na virusi hivyo.
Raia wa Afrika Kusini, kwa wiki ya tano sasa, wameendelea kusalia nyumbani katika vita dhidi ya mamabukizi hayo, hatua ambayo serikali nchini humo inasema imesaidia kupunguza maambukizi hayo.