DRC-KAMERHE-UCHUMI-HAKI

Kesi ya Kamerhe kurejelewa Jumatano wiki ijayo

Vital Kamerhe alikuwa akisimamia mpango wa dharura wa siku 100 ambao umemtia matatani na kutuhumiwa matumizi mabaya ya fedha za umaa.
Vital Kamerhe alikuwa akisimamia mpango wa dharura wa siku 100 ambao umemtia matatani na kutuhumiwa matumizi mabaya ya fedha za umaa. REUTERS/Baz Ratner

Kesi ya aliyekuwa mnadhimu mkuu katika Ofisi ya rais jijini Kinshasa Vital Kamerhe inatarajiwa kurejelewa tena Jumatano Juni 3, 2020, kulingana na vyanzo vya mahakama.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo unakuja saa chache baada ya kifo cha mkuu wa mahakama ya mwanzo ya Gombe jijini Kinshasa, Raphael Yanyi, aliyefariki ghafla usiku wa Jumanne kuamkiwa Jumatano wiki hii mjini Kinshasa.

Kifo cha jaji anayesimamia kesi ya Vital Kamerhe, aliyekuwa mnadhimu mkuu katika Ofisi ya rais Feliox Tshisekedi, jijini Kinshasa kimewashangaza wengi nchini DRC.

Familia yake na mashirika yanayotetea haki za binadamu nchini DRC yameomba mwili wa Raphael Yanyi ufanyiwe uchunguzi na vipimo mbalimbali ili kujua kwamba aliuawa au ni kifo cha kawaida.

Katika kesi ya hivi karibuni ambayo ilisikilizwa kwa dakika chache na baadaye kuahirishwa, Vital Kamerhe alikanusha madai ya kutumia vibaya zaidi ya dola milioni 50 za Kimarekani zilizokuwa zimetengwa kugharamia ujenzi wa makaazi ya polisi na maafisa wa jeshi jijini Kinshasa wakati kesi yake iliporejelewa Jumatatu Mei 25.

Akijibu baadhi ya maswali ya majaji kuhusu mikataba ya ununuzi wa nyumba kutoka kampuni ya Samibo inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Lebanon, Samih Jamal, Vital Kamerhe alisema baadhi ya mikataba ilisainiwa bila ya yeye kupewa taarifa.