DRC-BENI-SIASA-USALAMA

DRC: Meya wa jiji la Beni afutwa kazi

Buanakawa Masumbuko Nyoni, Meya wa mji wa Beni, katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amefutwa kazi baada ya kutoa kauli ambayo haikufurahisha mamlaka ya mkoa huo.

Moja ya mitaa ya mji wa Beni ambako maandamano yalifanyika, Machi 2019.
Moja ya mitaa ya mji wa Beni ambako maandamano yalifanyika, Machi 2019. ALEXIS HUGUET / AFP
Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni Buanakawa Masumbuko Nyoni aliwashutumu hadharani viongozi wa mkoa kwamba wanahusika kwa ukosefu wa usalama katika mji wa Beni. Meya huyo alikuwa akizungumzia kuhusu kuongezeka kwa uhalifu na mauaji katikamji wa Beni. Lakini, kwa upande wa wakazi wa mji huo, wanasema meya huyo hawajibiki kwa majukumu yake.

Buanakawa Masumbuko Nyoni, Meya wa mji wa Beni alishtumu mamlaka ya mkoa na pia wabunge katika ngazi ya mkoa na wale katika ngazi ya kitaifa kwamba wanahusika kwa ukosefu wa usalama katika mji wa Beni. Maneno ambayo aliyasemea kwenye radio moja ya mji huo.

Watu wanaovalia sare za vikosi vya usalama na ulizi wameonekana wakiwatishia usalama raia wasiokuwa na hatia katikati mwa jiji, wakala msambazaji wa vocha kupitia simu za mkononi na watu wengine wawili waliuawa jioni. Na, katika maandamano ya amani yaliyoandaliwa na shirika la kiraia la Lucha kwa kulaani ukosefu huu wa usalama, Billy Kambale, mwanaharakati ambaye alikuwa bado kijana, aliuawa kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi mchana kweupe. Maandamano ya raia yaligeuka na kumtaka meya wa mji aw Beni kujiuzulu.

Mbale, mkazi wa Beni, amesema meya wa mji wa Beni hakuwajibika kwa kazi yake. Ambebaini kwamba, baada ya kuwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi, imeonekaa kuwa kazi ya Buanakawa Nyonyi haikuwa nzuri .

Kwa upande wake Buanakawa Nyonyi, amesema maamdamano hayo yaliandaliwa ili kupaka tope kwa lengo la kumtimuwa kwenye wadhifa wake.

Katika agizo la kusimamishwa kazi, gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini alibaini kwamba meya wa mji wa Beni alishindwa kujizuia katika taarifa zake, vile vile na "vitendo vya kupindukia" na kuweka hatarini mamlaka ya serikali.