Kamerhe kufikishwa tena mahakamani Jumatano wiki hii
Imechapishwa:
Kesi ya aliyekuwa mnadhimu mkuu katika Ofisi ya rais jijini Kinshasa Vital Kamerhe inatarajiwa kurejelewa tena Jumatano Juni 3, 2020, kulingana na vyanzo vya mahakama.
Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya kifo cha mkuu wa mahakama ya mwanzo ya Gombe jijini Kinshasa, Raphael Yanyi, aliyefariki ghafla usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano wiki iliyopita mjini Kinshasa.
Kifo cha jaji anayesimamia kesi ya Vital Kamerhe, aliyekuwa mnadhimu mkuu katika Ofisi ya rais Felix Tshisekedi, jijini Kinshasa kiliwashangaza wengi nchini DRC.
Familia yake na mashirika yanayotetea haki za binadamu nchini DRC yameomba mwili wa Raphael Yanyi ufanyiwe uchunguzi na vipimo mbalimbali ili kujua kwamba aliuawa au ni kifo cha kawaida.
Katika kesi ya hivi karibuni ambayo ilisikilizwa kwa dakika chache na baadaye kuahirishwa, Vital Kamerhe alikanusha madai ya kutumia vibaya zaidi ya dola milioni 50 za Kimarekani zilizokuwa zimetengwa kugharamia ujenzi wa makaazi ya polisi na maafisa wa jeshi jijini Kinshasa wakati kesi yake iliporejelewa Jumatatu Mei 25.
Akijibu baadhi ya maswali ya majaji kuhusu mikataba ya ununuzi wa nyumba kutoka kampuni ya Samibo inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Lebanon, Samih Jamal, Vital Kamerhe alisema baadhi ya mikataba ilisainiwa bila ya yeye kupewa taarifa.