MSUMBIJI-USALAMA

Shambulio la wanajihadi lazimwa Msumbiji

Kijiji cha Aldeia da Paz, karibu na Macomia katika mkoa wa Cabo Delgado, baada ya shambulio la kigaidi, Agosti 2019.
Kijiji cha Aldeia da Paz, karibu na Macomia katika mkoa wa Cabo Delgado, baada ya shambulio la kigaidi, Agosti 2019. MARCO LONGARI / AFP

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi mwishoni mwa wiki hii alitangaza kwamba walifanikiwa kuzima shambulio kubwa la wanamgambo wa Kiislamu katika mji wa Macomia wiki iliyopita, mji mkuu wa wilaya moja ya mkoa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi.

Matangazo ya kibiashara

Nyusi pia alitangaza vifo vya wamgambo kadhaa wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na maafisa wakuu wawili.

Tangu mwezi Machi mwaka huu, wanamgambo wa Kiislamu wanaendelea na mashambulizi katika mkoa wa Cabo Delgado. pia wamefanikiwa kudhibiti miji mitatu muhimu, miji mikuu kadhaa ya wilaya.

Usiku wa Jumatano kuakia Alhamisi wiki iliyopita, walijaribu kudhibiti mji mkuu wa nne, mji wa Macomia. Na baada ya siku tatu za mapigano, hatimaye vikosi vya serikali viliuweka kwenye himaya yao. Baada ya hapo viongozi walitangaza vifo vya wanamgambo 78 wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na maafisa wakuu wawili waliokuwa wakiongoza kundi la waasi.

Ushindi huu ni muhimu, kwa mujibu wa Eric Morier-Genoud, profesa wa historia ya Afrika katika chuo kikuu cha Queen's University huko Belfast na mtaalam nchini Msumbiji. Kwa sababu licha ya ahadi za rais Filipe Nyusi, jeshi la Msumbiji na polisi hadi sasa wamekuwa wameonekana kuwa hawawezi kurejesha utulivu. Mtafiti huyo amebaini kwamba serikali inakodi mamluki kutoka Afrika Kusini wakiwa wamejihami kwa helikopta na labda ndege zisizo kuwa na rubani, msaada wao umefanya jambo muhimu.

Lakini mapambano yanaendelea. Kwa sababu ndani ya kipindi cha miezi miwili, Wanajihadi walifanikiwa kudhibiti maeneo mengi. Sasa wanadhibiti nusu ya mkoa wa Cabo Delgado.

Kwa zaidi ya miaka miwili, kundi la wanamgambo wa Kiislamu kutoka nchini humo lililojiunga hivi karibuni na kundila Islamic State kwa jina la "al-Shabab" limeendelmea kuhatarisha usalama katika mkoa huo duni lakini wenye utajiri mkubwa wa gesi.

Machafuko katika mkoa huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100, ikiwa ni pamoja na raia 700, kulingana na ripoti ya shirika lisilo kuwa la kiserikali la Armed Conflict Location and Event Data Project (Acled). Watu wasiopungua 150,000 waliyatoroka makazi yao, mamlaka zimesema.