SOMALIA-UN-USALAMA-MAJANGA YA ASILI

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Somalia

Dereva wa gari hili akikabiliwa na wingu la nzige wa jangwani nje ya jiji la Dusamareb katika mkoa wa Galmudug, Somalia, Desemba 22, 2019.
Dereva wa gari hili akikabiliwa na wingu la nzige wa jangwani nje ya jiji la Dusamareb katika mkoa wa Galmudug, Somalia, Desemba 22, 2019. REUTERS/Feisal Omar/File Photo

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na utoaji wa misaada ya kibinadamu nchini Somalia, linasema kuwa utulivu wa kisiasa na amani ambao umekuwepo nchini humo kwa muda wa miaka kumi iliyopita, huenda ukazoroteshwa na mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na ugonjwa wa Corona.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa shirika hilo, Justin Brady, akiongea mjini Mogadishu, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Somalia katika kukabiliana na mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na ugonjwa hatari wa Corona.

“Pigo la matatizo hayo matatu si tu la kibinadamu bali linaweza kuvuruga maendeleo ya kisiasa na usalama nchini Somalia. Lazima tushirikiane na jamii ya kimataifa kwa kuitoa nchi ya Somalia katika matatizo hayo, “ Justin Brady amesema.

“Tayari tumewapa waliokumbwa na matatizo hayo matatu makaazi na pia  tumewapa mahitaji mengine ya dharura. Tumechukua hatua kuhakikisha kuwa tunazuia kuenea kwa magonjwa ya kuhara, kipindupindu na utapia mlo, magonjwa ambayo husababishwa na mafuriko, “ Bw. Brady ameongeza.

“Mafuriko yalikuwa kwenye sehemu za biashara na masoko na kuwaacha watu wengi bila namna ya kupata mahitaji yao ya kila siku. Bei za bidhaa sasa zimepanda. Mazao yaliyokuwa tayari kuondolewa mashambani yaliharibiwa na mafuriko, “ amebaini Hussein Abdi, kiongozi wa shirika lisilo la serikali  nchini Somalia la Development Action Network.

Mwakilishi wa shirika la Afya Duniani nchini Somalia, Dkt Mamunur Rahman Malik, amesema kuwa ikiwa Somalia haitapata misaada ya kifedha kutoka jumuiya ya kimataifa, itakuwa vigumu kukabiliana na mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na ugonjwa wa Corona.

“Hapa Somalia tuna visa  vingi vya Corona ambavyo havijafanyiwa uchunguzi, na havijagunduliwa na hali ya watu kubakia katika karantini haitekelezwi. Kilichotokea ni kusambazwa kwa virusi vya Corona, “ amesema Dkt Mamunur Rahman.

Kufikia Alhamisi wiki hii, Somalia imerekodi zaidi ya visa elfu-mbili vya ugonjwa wa Corona na vifo sabini-na-tisa.

Hali kadhalika, zaidi ya watu nusu milioni wameachwa bila makaazi kutokana na mafuriko.

Licha ya uvamizi wa nzige wa jangwani na kuzuka kwa ugonjwa wa Corona, Somalia imekumbwa na mdororo wa usalama unaotokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Al Shabab, na kutozalisha chakula kumesababisha njaa kubwa kwa muda wa miaka mingi.