AFRIKA KUSINI-MAREKANI-USALAMA

ANC yalaani mauaji ya George Floyd Marekani

Cyril Ramaphosa amelaani mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd nchini Marekani.
Cyril Ramaphosa amelaani mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd nchini Marekani. REUTERS/Rodger Bosch

Chama tawala nchini Afrika Kusini ANC, kinazindua kampeni inayofahamika kama Ijumaa nyeusi, kulaani ubaguzi wa rangi baada ya kuuawa kwa mwanamume mweusi George Floyd  mikononi mwa polisi mzungu mwezi uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa amezindua kampeni hiyo, ambayo itawataka watu nchini humo kuvalia mavazi meusi kila Ijumaa ili kulaani mauaji yaliyotokea nchini Marekani na kupinga visa vya ubaguzi wa rangi.

Kampeni hii pia inatarajiwa kuwakumbuka raia wa nchi hiyo ambao wamepoteza maisha mikononi mwa maafisa wa polisi katika taifa hilo ambalo pia limekuwa na historia ya ubaguzi wa rangi.

Siku ya Jumatano, maandamano yalishuhudiwa jijini Cape Town, kulaani mauaji ya George Floyd maandamano ambayo pia yalishuhudiwa nje ya ubalozi wa Marekani jijini Nairobi nchini Kenya wiki hii.

Viongozi wengine wa bara Afrika wakiongozwa na rais wa Ghana Nana Kuffo Addo, wamejitokeza na kulaani mauaji hayo, na kusema yanashtua na hayakubaliki, ujumbe ambao pia umetolewa na Umoja wa Afrika.