DRC: Vital Kamerhe akanusha madai dhidi yake
Imechapishwa:
Kesi inayomhusisha Vital Kamerhe, mkurugenzi wa Ofisi ya rais Félix Tshisekedi, na washitakiwa wengine wawili imeendelea kusikilizwa alhamisi wiki hii kwa siku mbili mfululizo katika gereza kuu la Makala, jijini Kinshasa.
Kesi hii inahusu uratibu wa fedha zilizokuwa zimetengwa kugharamia ujenzi wa makaazi ya polisi na maafisa wa jeshi jijini Kinshasa kama sehemu ya mpango wa siku 100 wa rais Félix Tshisekedi.
Kwa mara ya kwanza Jumatano hii, mashahidi walisikilizwa katika kesi hiyo. Waziri wa zamani wa Maendeleo Vijijini Justin Bitakwira ni miongoni mwa mashahidi waliosikiliwza.
Justin Bitakwira ndiye ambaye alisaini mkataba wa awali mwaka 2018 na kampuni ya Samibo SARL ya mfanyabiashara wa Lebanon Samih Jammal, ambaye pia ni miongoni mwa washtakiwa.
Amebaini kwamba hapo awali ilikuwa mkataba wa karibu dola milioni 27 kwa ujenzi wa nyumba 900 zilizotengwa kwa mikoa 9 kote nchini.
Justin Bitakwira alikubali kuwa alitia saini kwenye mkataba huo. Lakini alibaini kwamba serikali haikuweza kulipa awamu ya kwanza ya malipo kwa kampuni ya Samibo SARL wakati huo. Aliongeza kuwa hakuweza kufuatilia suala hilo kwa sababu alikuwa ameondolewa na Vital Kamerhe kupitia barua rasmi. "Wakati rais Félix Tshisekedi alichukuwa hatamu ya uongozi wa nchi, Kamerhe alizorotesgha serikali yetu. Tulifika tunakuwa kama watazamaji, "alisema mbele ya mahakama.
Amemshtumu mkurugenzi wa ofisi ya rais Felix Tshisekedi, na kuongeza kuwa hana taarifa kuhusu malipo ya dola milioni 57 kwa kampuni ya Samibo SARL. Kiwango hiki ni tofauti na kile cha dola milioni 27 katika mkataba wa awali.
"Sijawahi kusiani mkataba wowote wa DRC kulipa dola milioni 57. Yule ambaye alifanya hivyo aje akubali mwenyewe hapa, " alisema Justin Bitakwira.
Maneno haya yameungwa mkono na ushuhuda wa Ngongo Salumu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa Umma, shahidi wa mwisho anatarajiwa kusikilizwa leo Alhamisi. Shahidi huyu pia amesema kwamba malipo hayo yalifanywa kwa msingi wa hati isiyo halali.
Marcellin Bilomba, mshauri mkuu wa rais katika maswala ya kiuchumi, amesema mbele ya majaji kwamba dola 66,700,000 zilililipwa kampuni Samibo SARL kwa ujenzi wa nyumba 1,500.
Hata hivyo Kamerhe amekanusha madai hayo akisema kuwa alichukuwa uammuzi chini ya agizo ya rais Tshisekedi.