Mwendesha mashitaka wa ICC aonya kuhusu machafuko Ituri
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mwendesha mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, Fatou Bensouda amezitaka mamlaka za DRC kutafutia ufumbuzi kuhusu kudorora kwa usalama nchini humo.
Fatou BenSouda pia ameonya wanamgambo wa kundi la CODECO kuhusu machafuko yanayoendelea huko Ituri, Kaskazini Mashariki mwa DRC.
Amesema ikiwa hali ya mgogoro wa kiafya inayosababishwa na janga la Corona itadhibitiwa, maafisa wake wa uchunguzi watazuru mkoa wa Ituri kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu vinavyodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa CODECO na makundi mengine yenye silaha katika mkoa huo.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetangaza vifo vya raia 1,300 katika miezi nane iliyopita nchini DRC.
Katika taarifa yake, Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, ameeleza kwamba baadhi ya matukio yaliyohusisha mauaji na uhalifu mwingine na ukiukwaji vinaweza kusababisha uhalifu dhidi ya binadamu au uhalifu wa kivita
Umoja wa Mataifa pia umebaini kwamba zaidi ya watu 510,000 wamelazimika kuyatoroka makaazi yao kufuatia machafuko katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini katika kipindi cha miezi tisa.