Maporomoko ya udongo yaua karibu watu 13 Côte d'Ivoire
Imechapishwa:
Watu 13 wamefariki dunia na wengine wengi hawajulikani waliko kufuatia kisa cha maporomoko ya udongo huko Anyama, katika moja ya viunga vya Kaskazini mwa mji wa Abidjan, nchini Côte d'Ivoire.
Wakati huo huo nyumba kadhaa zimeboka kutokana na maporomoko hayo ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha katika siku za hivi karibuni.
Kulingana na duru za kuaminika, watoto kadhaa wamefariki dunia na wengine hawajulikani waliko mpaka sasa, ambapo shughuli ya uokoaji inaendelea.
"Nimempoteza mtoto wangu wa miaka mitatu, natafuta mwili wake. Sina tena matumaini ya kumpata akiwa hai," Aboubacar Dagnon, mkaazi wa wa eneo la Anyama ameliambia shirika la habari la AFP. Hakuwapo wakati wa janga hilo, lakini nyumba ya mke wake, ambaye alinusurika, ilifunikwa na udongo na amekuwa akiendelea kutafuta mwanae chini ya chini ya vifusi vya nyumba za majirani.
Mamia ya watu, ambao baadhi yao wakati mwingine huzama na kufikia hadi kwenye magoti au hata kwenye viuno ndani ya matope, wanajaribu kuwatafuta watu ambao bado wako hai,huku baadhi ya vitu kama sufuria, milango, nyaraka, nguo na viatu vikiokotwa kutoka chini ya ardhi kwenye urefu wa kina cha zaidi ya mita 70.
"Watu kumi na tatu wamekufa, hii ni ripoti ya awali, laikini zoezi la kutafuta miili mingine linaendelea," mkuu wa mkoa wa Abidjan, Vincent Toh Bi amesema.
Hata hivyo maafisa wa idara inayokabiliana na majanga wamesema kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.