Machafuko yawalazimu watu zaidi ya milioni kutoroka makazi yao mashariki mwa DRC
Zaidi ya watu milioni Moja wamelazimika kutoroka makazi yao nchini DRC kufwatia ghasia na mapigano ya mara kwa mara katika miezi sita iliyopita, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa anayeshughulikia Wakimbizi (UNHCR) amesema.
Imechapishwa:
Katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari jumanne hii ya june 30 shirika hilo la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limefahamisha kuwa limesikitishwa na ongezeko la mapigano, mauaji, na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyotendewa raia waishio mashariki mwa taifa hilo na hivyo kuomba kupelekwa kwa wanajeshi wa Serikali, FARDC, lakini pia polisi wakisaidiwa na Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, Monusco katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi.
Hata hivyo, wanaharakati huko DRC wamefahamisha kuwa maafisa wa jeshi la serikali na Polisi ni miongoni mwa wale wanaohusika kwa njia moja ama nyingine katika visa vya ukiukaji wa Haki za binadamu, uporaji na wizi wa mali ya raia kwenye eneo hilo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika kipindi cha wiki nane zilizopita, UNHCR na washirika wake wamesema kuwa wamerekodi mashambulio mengi yaliyotekelezwa na wapiganaji wenye silaha huko Djugu katika mkoa wa Ituri, hali kadhalika huko Fizi na Mwenga mkoani Kivu Kusini, lakini pia wilayani Masisi na Rutshuru mkoani Kivu Kaskazini, yote haya yametokea Mashariki mwa nchi hiyo.