DRC-UBELGIJI-USHIRIKIANO

Wakongo wakaribisha maneno ya Mfalme Philippe kuhusu ukoloni dhidi ya Congo DRC

Mfalme wa Ubelgiji Philippe kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo amewasilisha masikitiko yake ya kina ya majeraha yaliyosababishwa wakati wa ukoloni wa Ubelgiji nchini DRC, barua aliyomtumia Rais wa nchi katika fursa ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa nchi hiyo.

Rais wa Kongo Félix Tshisekedi akiwa na Mfalme wa wa Ubelgiji, Mfalme Philippe, kwenye kasri ya kifalme huko Brussels, Septemba 17, 2019.
Rais wa Kongo Félix Tshisekedi akiwa na Mfalme wa wa Ubelgiji, Mfalme Philippe, kwenye kasri ya kifalme huko Brussels, Septemba 17, 2019. REUTERS/Francois Lenoir
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Marie-Ntumba Nzeza, amekaribisha kwanza msimamo wa Mfalme philippe kwa kutambuwa kuwa mwananchi wa DRC "hakuchukuliwa kwa heshima ya hadhi ya binadamu". "Haya ni maneno mazuri ambayo DRC na wananchi wake wanaweza kupongeza, " amesema Waziri Marie-Ntumba Nzeza.

"Wananchi wa DRC wameridhika kwa kile walichokuwa wanasubiri kutoka Ubelgiji. Hatu hii itaimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa yetu mawili. Pia ni msingi wenye nguvu ya kijamii na kisaikolojia ambao utabadilisha mtazamo wetu sisi wenyewe. Ubelgiji na Mfalme Philippe wameweka misingi ya mageuzi makubwa, " Waziri Marie-Ntumba Nzeza ameongeza.

Kwa upande wa Carbone Beni kutoka shirika la kiraia Filimbi, amesema hatua hiyo Mfalme Philippe na Ubelgiji pia ni "msimamo wa kihistoria", lakini hawapaswi kuishia hapo. Ameomba historia hii ya pamoja ifundishwe katika nchi zote mbili.

Bienvenu Matumo kutoka shirika la kiraia la Lucha, lamesema kwa upande wake, Ubelgiji bado na hatua kadhaa za kuchukua. "Kuna uhalifu mwingi wa kiuchumi, lakini pia ukiukwaji wa haki za binadamu ambao umefanywa nchini DRC na Leopold na utawala wa ukoloni wa Ubelgiji. Lazima tuangalie utaratibu wa kukarabati ambao unaweza kuwa msingi wa uhusiano wetu mpya na Ubelgiji."

Bienvenu Matumo anasema mbali na kuelezea masikitiko yake, lakini pia msamaha wa kweli unahitajika.

Mtu anayekiri makosa, anaomba msamaha, tayari ni jambo la msingi. jambo muhimu kwa hilo , kwanza sio yeye aliyetekeleza makosa hayo! Sisi ni kizazi cha baada ya miongo kadhaa ya ukoloni huo, maneneo ya Mfalme Philippe ni ya kutia moyo.

Wanahistoria wanasema mamilioni ya Wakongo waliuawa, kukatwa viungo vyao ama kufa kwa maradhi wakati wakifanyishwa kazi za suruba kwenye mashamba ya mipira yaliyokuwa yakimilikiwa na Mfalme Leopold II wa Ubelgiji. Bila ya kumtaja babu yake huyo mkuu kwa jina, Mfalme Philippe ameandika kwenye barua hiyo kwamba matendo ya ukatili na unyama yaliyofanywa wakati huo ni sehemu kubwa ya kumbukumbu za pamoja kati ya Congo na Ubelgiji.

Sanamu kadhaa za Leopold II, aliyetawala kati ya mwaka 1865 na 1909, zimechafuliwa kwa rangi au kuvunjwa na waandamanaji nchini Ubelgiji katika siku za hivi karibuni, hasa katika wimbi la hasira kubwa iliyochochewa na mauaji ya George Floyd mmarekani mweusi mwezi uliopita katika mikononi mwa polisi wa Minneapolis, Marekani. Suala ambalo bado linaendelea kuleta vurugu na machfuko nchini humo na kwingineko.