DRC-USALAMA

DRC: Ituri yakumbwa na machafuko mapya

Ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (UNJHRO) mapema wiki hii iliripoti kuongezeka kwa visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika jimbo la Ituri.

Walinda amani wa Monusco wakipiga doria katika mitaa ya eneo la Djugu, katika mkoa wa Ituri, Machi 13, 2020.
Walinda amani wa Monusco wakipiga doria katika mitaa ya eneo la Djugu, katika mkoa wa Ituri, Machi 13, 2020. SAMIR TOUNSI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Kama ilivyo mwezi uliopita, makundi ya watu wenye silaha ndio sababu kuu ya machafuko yaliyoorodheshwa katika mkoa huo wa Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Askari wengi wametumwa kusaidi vikosi vingine vinavyosimamia amani katika mkoa huo unaoendelea kukumbwa na vitisho mbalimbali.

Moja ya vitisho hivyo vimeshuhudiwa katika eneo la Aru kilomita kadhaa na mpaka wa Uganda na Sudani Kusini. Tangu mwezi Aprili, angalau matukio saba ya jeshi la Sudani Kusini kuingia katika ardhi ya DRC yameorodheshwa na majeshi ya DRC. Wanajeshi wa Sudani Kusini wamekuwa wakiwatimuwa mara kwa mara waasi wa nchi hiyo hadi katika ardhi ya DRC. Visa vya uporaji na nyumba kuchomwa vimeripotiwa na vyanzo kadhaa katika eneo hilo.

Askari wengi wametumwa katika eneo la Aru ili kuimarisha usalama na kuzingira eneo lote la mpaka na nchi hizo mbili kwa kuhofia hali ya usalama kuzorota zaidi.

Wakati huo kamati ya ulinzi ya Bunge iliiagiza serikali wiki hii kuimarisha uwezo wa majeshi ya FARDC kwa kuunda kitengo maalum kitakachohusika na ulinzi wa mipaka.

Katika eneo la Irumu, operesheni za pamoja zimekuwa zinaendeshwa na askari walio katika mkoa jirani wa Kivu Kaskazini tangu wiki iliyopita, kwa lengo la kupambana na kundi la wanamgambo wa Maï-Maï. Changamoto nyingine bado ni uvamizi wa mara kwa mara wa wapiganaji wa kundi la waasi wa Uganda la ADF kutoka wilaya ya Beni. Kuna pia wilaya za Mahagi na Djugu, ambapo jeshi limekuwa kilikabiliana na mashambulizi kadhaa dhidi ya raia, yanayotekelezwa na kundi la wanamgambo wa CODECO.

Mbali na hatua hizi za kijeshi, serikali inatarajia kuanza mchakato wa kuhamasisha wapiganaji, raia wa DRC katika maeneo hayo ili waweze kurejeshwa katika maisha ya kiraia na wengine waingizwe katikia jeshi na polisi. Ujumbe wa viongozi wa zamani wa waasi, maafisa kutoka Ituri, waliwasili wiki hii katika mkoa huo ili kuanzisha mara moja mchakato huo.