CHAD-G5 SAHEL-USALAMA

G5 Sahel: Idriss Déby ataka jeshi lake libaki Chad

Rais wa Chad Idriss Déby katika mkutano wa kilele wa G5 Sahel, Juni 30, 2020.
Rais wa Chad Idriss Déby katika mkutano wa kilele wa G5 Sahel, Juni 30, 2020. Ludovic Marin /Pool via REUTERS

Rais wa Chad Idriss Deby katika mkutano wa G5 Sahel uliofanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, alisisitiza kuwa anapendelea kuona jeshi lake linabaki nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya rais wa Chad imezua wasiwasi na kubaini kwamba rais Idriss Deby hataki kushirikiana na mataifa mengine ya G5 Sahel katika kutuma majeshi yao ili kusimamia amani katika eneo hilo ambalo linakumbwa na mashambulizi ya makundi yenye silaha.

Katika mkutano wa nchi hizo uliofanyika katika mji wa Pau mwezi Januari mwaka huu, viongozi kutoka nchi hizo na washirika wao waliafikiana kutuma majeshi kwenye mipaka ya nchi tatu za ukanda huo ili kukabiliana na makundi yenye silaha yanayohatarisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Rais wa Chad alibaini kwamba hali ya usalama si shwari nchini mwake.

"Tishio karibu na Ziwa Chad bado linaendelea kuongezeka na maji yameongezeka. Hoja zozote zile kuhusu kutumwa kwa jeshi la Chad nje ya nchi hazitakubaliwa kwa usalama wa Chad, "Idriss Déby alisema katika mkutano wa kilele wa G5 Sahel uliofanyika siku za hivi karibuni huko Nouakchott.

Tayari Aprili 10, rais wa Chad alihakikishia kwamba "hakuna mwanajeshi wa nchi yake atayeshiriki [katika] operesheni ya jeshi nje ya Chad". Mwishoni mwa mwezi Machi, askari 480 waliokuwa wametumwa kushiriki katika kikosi cha kimataifa kutoa ulinzi wa maeneo matatu ya mpakani, walirejeshwa wakiwa njiani kushiriki katika peresheni iliyoitwa "hasira za Bohoma", kujibu shambulio la Boko Haram ambalo liligharimu maisha ya mamia ya wanajeshi wa Chad Machi 23.

Hata hivyo Ufaransa bado ina matumaini kwamba Chad itatekeleza ahadi yake ya kutuma kikosi hicho kwenye maeneo hayo ya mipaka.