DRC-SIASA-USALAMA-UHURU

Vuguvugu lisilofahamika lataka kuwepo na jamhuri inayojitawala ya Kivu

Mji wa Bukavu, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kusini.
Mji wa Bukavu, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kusini. Wikimedia/EMMANRMS

Wakaazi wa  mji wa Bukavu Mashariki mwa DRC tarehe 1 mwezi huu waliamka kwa mshangao na kukuta mji wao umepambwa na bendera mpya inayoaminiwa kusimikwa na vuguvuvugu linalotaka kujitenga na kuunda nchi yao ya Jamhuri ya Kivu.

Matangazo ya kibiashara

Bendera hiyo ilikuwa na rangi tatu, ya njano, nyeusi na samawati. Hii ni mara ya kwanza hali hii kushuhudiwa Mashariki mwa nchi hiyo, kujitokeza vuguvugu linalotaka kujitenga.

Tukio hili limewashangaza wengi na hadi sasa vuguvugu linalodai kujitenga na kuunda nchi ya Kivu bado halijafahamika.

Hata hivyo, nyaraka ambayo haikuwa imetiwa saini, ilionesha majina ya watu mashuhuri kutoka eneo la Kivu, wakiongozwa na Gavana wa zamani wa jimbo la Kivu Kusini Marcelin Tchishambo, kama kiongozi pamoja na orodha ya Mawaziri Wake 19.

Miongoni mwa majina yaliyotajwa ni mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel, Daktari Dennis Mukwege, ambaye amejitiokeza na kukana kufahamu chochote kuhusu mpango huo na kudai wanaofanya harakati hizo wana lengo la kuwagawanya wananchi wa Kivu.

“Nawaonya watu wetu wasidanayike na kunaswa na mtego huu unaodai uhuru wa Kivu. Watu hawa kwa miaka 25 wamekuwa wakishirikiana na watu kutoka nje kuendelea kusababisha mateso kwa watu wetu. Lengo ni kutugawa, ili waendelee kuchukua rasimali zetu na kutufanya sisi kuwa watumwa, “ amesema Daktari Dennis Mukwege.

Hata hivyo, bendera hizo ziliondolewa haraka  na maafisa wa usalama jijini Bukavu.

Rais Felix Tshisekedi kwenye kikao chake cha Mawaziri Ijumaa ya wiki iliyopita, alionesha masikitiko yake na kuagiza maafisa wa usalama kufanya uchunguzi wa kina na kuwafubgulia mashitaka wote waliohusika.