MADAGASCAR-CORONA-AFYA

Coronavirus: Madagascar yachukua tena hatua za kudhibiti maambukizi

Rais Andry Rajoelina alizindua dawa ya Covid Organics, inayotokana na mmea unaotibu malaria na kuuthibitishia ulimwengu kuwa inaponya ugonjwa wa Corona, lakini hadi sasa haijathibitishwa na shirika la afya duniani WHO, na pia utafiti wowote wa kisayansi.
Rais Andry Rajoelina alizindua dawa ya Covid Organics, inayotokana na mmea unaotibu malaria na kuuthibitishia ulimwengu kuwa inaponya ugonjwa wa Corona, lakini hadi sasa haijathibitishwa na shirika la afya duniani WHO, na pia utafiti wowote wa kisayansi. © AFP / Rijasolo

Serikali ya Madagascar imetangaza kurejelewa tena kwa amri ya kutotembea kufuatia ongezeko jipya la maambukizi ya virusi vya Corona, miezi miwili baada ya masharti hayo kuondolewa.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina aliitangaza hatua hiyo hivi majuzi baada ya nchi hiyo kushuhudia ongezeko jipya la visa vya maambukizi ya virusi vya Corona, baada ya miezi miwili tu kupita ambapo serikali hiyo ilikuwa imeondoa amri ya watu kutotembea kama sehemu ya kuzuia maambukizi hayo ya Corona.

Wizara ya Afya nchini humo imelitaja eneo la Analamanga kuwa lenye maambukizi zaidi, ambako serikali imesema kuanzia sasa ni mtu mmoja mmoja katika kila familia atakayeruhusiwa kutoka nje kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa sita mchana, masharti ambayo yataendelea kuzingatiwa hadi Julai 20, limesema tangazo la serikali ya Antananarivo.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Corona, mwezi Macih Madagascar ina wagonjwa 2,728, huku watu 29 walikufa kutokana na ugonjwa huo kufikia siku ya Jumapili iliyopita.

Mwezi Aprili nchi ya Madagascar ilizindua dawa ya mitishamba "Covid Organics", inayotokana na mmea unaotibu Malaria na kuuthibitishia ulimwengu kuwa inaponya ugonjwa wa Corona, lakini hadi sasa haijathibitishwa na shirika la Afya Duniani WHO, na pia utafiti wowote wa kisayansi.