MALI-SIASA-USALAMA

Rais wa Mali ajaribu kutuliza mvutano unaoendelea

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta.
Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta. Issouf Sanogo/AFP

Rais wa Mali Ibrahim Boubakar Keita amesema kwamba angeweza kuwateua wagombea ambao hawakufanikiwa katika uchaguzi wa maseneta katika uchaguzi wa hivi karibuni ili kurejesha hali ya utulivu, kauli ambayo ameitoa baada ya nchi yake kushuhudia majuma kadhaa ya maandamano ya upinzani.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya rais wa Mali IBK, Ibrahim Boubakar Keita inakuja siku moja baada ya kiongozi huyo kukutana kwa mazungumzo na kinara wa upinzani Sheikh Mahmoud Dicko ambaye amefanikiwa kuongoza maelfu ya waandamanaji mitaani kupinga serikali ya nchi hiyo.

Huo ni mkutano wa kwanza rasmi kufanyika baina ya watu hao wawili tangu maandamano mawili kufanyika yakionesha jinsi wananchi wa Mali hawaridhishwi na utendaji wa serikali ya Rais Keita, hasa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha yaliyosababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mamia ya melfu ya wengine kukimbia makazi yao tangu mwaka 2012

Rais Keita ameviambia vyombo vya habari kuwa lengo lake kuchukua uamuzi wa kuwateua wagombea ambao hawakufanikiwa katika uchaguzi wa maseneta wa hivi karibuni ni kujaribu kuwahamasisha wanasiasa wa upinzani kuchangia juhudi za upatikanaji wa amani na usalama kwenye taifa hilo.