Askari 23 waangamia katika shambulizi la watu wenye silaha Nigeria
Wapiganaji wa kijihadi nchini Nigeria, wamewauwa wanajeshi 23 katika shambulio la kushtukiza kwenye barabara kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Askari kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo.
Imechapishwa:
Taarifa kutoka idara ya usalama, zinasema wanajeshi hao walikuwa wanarejea kushika doria eneo la Maidugueri.
Mapema wiki watu waliojihami kwa silaha waliwauwa wakulima 15 Kaskazini Magharibi mwa Jimbo la Katsina, katika kile, polisi walitaja ni kisa cha wizi wa mifugo.
Nigeria ni moja ya nchi za Afrika Magharibi ambazo zinaendelea kukumbwa zaidi na utovu wa usalama kutokana na makundi mbalimbali yenye silaha, hasa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali, ikiwa ni pamoja na kundi la Boko Haram.
Mapema mwezi Juni watu wasiopungua hamsini waliuawa katika mashambulizi mawili yaliyotokea katika vijiji viwili, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, mauaji ambayo yalidaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State Afrika Magharibi (ISWAP).
Mashahidi wanasema watu waliojihami kwa silaha za kivita wakiwa katika magari walikabiliana na kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na serikali, lakini wanamgambo hao walizidiwa nguvu kutokana na idadi yao ndogo na hivyo kundi hasimu kutekeleza mauaji dhidi ya raia waliokuwa wakitoroka makazi yao, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.