MALI-SIASA-USALAMA

Mgogoro wa kisiasa nchini Mali: Rais IBK apendekeza kuifanyia marekebisho Mahakama ya Katiba

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta.
Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta. Issouf Sanogo/AFP

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta, ambaye anakabiliwa na upinzani mkubwa anaendelea kujaribu kutuliza joto la kisiasa linaloendelea kupanda nchini mwake.

Matangazo ya kibiashara

Usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Rais Keïta amelihutubia taifa na kupendekeza kufanyia marekebisho Mahakama ya Katiba.

Wengi nchini Mali wamekuwa wakikosoa Mahakama hiyo tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa wabunge.

Hii ni mara ya tatu Rais kulihutubia taifa tangu maandamano ya kwanza ya muungano wa vyama vya upinzani na mashirika mbalimbali, M5, kuandamana wakidai rais huyo ajiuzulu.

Tangu kujiuzulu kwa majaji wanne mapema mwezi Juni, mahakama hii ya juu nchini Mali imekumbwa na mgawanyiko mkubwa.

"Mahakama ya Katiba iitawapata wajumbe wapya katika muda wa saa au siku zijazo," Rais Keïta amesema, huku akikiri kwamba "uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuhusu matokeo ya uchaguzi umezusha na unaendelea kuzusha matatizo makubwa nchini.

Matokeo ya uchaguzi ya wabunge yalipingwa na sehemu raia wa Mali wakidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu.

Maandamano haya, katika miji kadhaa ya nchi, yalisababisha kuundwa kwa vuguvugu la M5, liloanzisha maandamano tangu mwanzoni mwa mwezi Juni. Maandamano ya tatu pia yamepangwa kufanyika kesho Ijumaa hii.