MALI-SIASA-USALAMA

Mali kukumbwa na maandamano makubwa

Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita.
Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita. REUTERS/Luc Gnago

Vuguvugu ambalo limekuwa likiongoza maandamano kumshinikiza rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu, limetangaza maandamano yao yataendelea kuanzia leo Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Hivi majuzi rais Boubacar alifanya mkutano na baadhi ya waandamanaji na kuahidi angewateuakwenye serikali yake, baadhi ya wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi uliopita, kama njia ya kurejesha hali ya utulivu.

Usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii Rais IBK alipendekeza kuifanyia marekebisho Mahakama ya Katiba.

Wengi nchini Mali wamekuwa wakikosoa Mahakama hiyo tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa wabunge.

Hii ni mara ya tatu Rais Keita kulihutubia taifa tangu maandamano ya kwanza ya muungano wa vyama vya upinzani na mashirika mbalimbali, M5, kuandamana wakidai rais huyo ajiuzulu.

Tangu kujiuzulu kwa majaji wanne mapema mwezi Juni, mahakama hii ya juu nchini Mali imekumbwa na mgawanyiko mkubwa.

"Mahakama ya Katiba itawapata wajumbe wapya katika muda wa saa au siku zijazo," Rais Keïta alisema, huku akikiri kwamba "uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuhusu matokeo ya uchaguzi umezusha na unaendelea kuzusha matatizo makubwa nchini.

Wadadisi wanasema hiyo ni mbinu ya Rais Ibrahim Boubacar Keïta, kujaribu kutuliza joto la kisiasa linaloendelea kupanda nchini mwake.

Matokeo ya uchaguzi ya wabunge yalipingwa na sehemu raia wa Mali wakidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu.

Maandamano haya, katika miji kadhaa ya nchi, yalisababisha kuundwa kwa vuguvugu la M5, liloanzisha maandamano tangu mwanzoni mwa mwezi Juni.