DRC-USALAMA

DRC: Kiongozi wa kundi la NDC-R avuliwa uongozi

Milio ya risasi ilisikika karibu na makao makuu ya NDC-R huko Pinga, katika Mkoa wa Kivu Kaskazini. (picha ya kumbukumbu)
Milio ya risasi ilisikika karibu na makao makuu ya NDC-R huko Pinga, katika Mkoa wa Kivu Kaskazini. (picha ya kumbukumbu) Photo: Monusco/ Ngwa Julius Nde

Kundi la wapiganaji la Nduma Defense of Congo-Rénové (NDC-R) linaloendesha harakati zake Mashariki mwa DRC limetangaza kwamba limemvua mamlaka ya uongozi kiongozi wake Guidon Shimiray.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na taarifa iliyosainiwa na msemaji wa kundi hilo, moja ya makundi makubwa nchini DRC, Guidon Shimiray anatuhumiwa "tabia ya kupotoka" kinyume na mapambano ya kundi hilo, "ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa na haki za binadamu".

Taarifa hii iliyotiwa saini Julai 8 imeelezea vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Guidon Shimiray mwaka 2018 na waranti wa kukamatwa uliotolewa na mahakama ya kijeshi ya Mkoa wa Kivu Kaskazini mwaka 2019.

Uongozi mpya wa kundi hili la NDC-R, uliokuwa ukisimamiwa hapo awali na naibu kiongozi, pia amesema yuko tayari kuweka chini silaha na kumuunga mkono Félix Tshisekedi.

Siku ya Alhamisi asubuhi, milio ya risasi ilisikika karibu na makao makuu ya kundi la NDC-R huko Pinga, mashariki mwa DRC. Kumeripotiwa watu waliouawa na wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo. Kulingana na vyanzo kadhaa, kulitokea mapigano kati ya uongozi mpya wa kundi hilo na wapiganaji ambao bado wanaomtii Guidon Shimiray.