MALI-SIASA-USALAMA

Makabiliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji yasababisha hasara Bamako

bamako manif barricades
bamako manif barricades AP Photo/Baba Ahmed

Hali ya sintofahamu inaendelea nchini Mali, wakati waandamanaji wanaendelea kuomba rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita ajiuzulu haraka iwezekanavyo.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano ya tatu ya vuguvugu la M5 dhidi ya rais wa Mali Ibarhim Boubacar Keita (IBK) Ijumaa wiki hii yalikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka vikosi vya ulinzi na usalama na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Vuguvugu la M5, lilianzishwa mapema mwezi Juni na linajumuisha sehemu ya mashirika ya kiraia, upinzani wa kisiasa na viongozi wa kidini.

Waandamanaji walivamia majengo kadhaa ya serikali ikiwa ni pamoja na makao makuu ya ORTM, Bunge la Kitaifa, na pia madaraja mawili huko Bamako.

Polisi iliingilia kati. Angalau mtu mmoja aliuawa na wengine 19 walijeruhiwa kwa risasi.

Maandamano yalianza baada ya sala kubwa ya Ijumaa, ingawa wakati wa adhuhuri kulikuwa na baadhi ya waandaaji na waandamanaji kwenye uwanja wa uhuru huko Bamako wakiwa na mabango yaliyoandikwa "IBK achia ngazi" au "Tunataka badiliko ". Vikosi vya ulinzi na usalama vilipelekwa, hasa kwenye barabara kuu, ameripoti mwandishi wetu huko Bamako, Serge Daniel.

Baada ya makao makuu ya shirika la utangazaji la ORTM kuvamiwa, televisheni ya taifa ilisitisha matangazo yake, kabla ya kurejeshwa hewani jioni.

Hata hivyo viongozi wa vuguvugu la M5 wameapa kuendelea na maandamano hadi pale watahakikisha rais IBK anaachia ngazi.