DRC-SIASA-USALAMA

DRC: Upinzani waapa kufanya maandamano jijini Kinshasa, polisi yaonya

Polisi imeonya watu watakaoitikia wito wa maandamano uliotolewa na muungano wa upinzani wa LAMUKA, DRC.
Polisi imeonya watu watakaoitikia wito wa maandamano uliotolewa na muungano wa upinzani wa LAMUKA, DRC. Alexis Huguet/AFP

Muungano wa upinzani nchini DRC wa  LAMUKA umetoa wito wa maandamano hivi leo kupinga uteuzi wa Ronsard Malonda kuwa mkuu wa Tume ya Uchaguzi ambae anasubiriwa kuidhinishwa na rais Felix Tshisekedi.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya Gavana wa jiji la Kinshasa kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, na licha ya vurugu zilizoshuhudiwa wiki iliopita  na kusababisha vifo kadhaa, upinzani huo umesisitiza juu ya kuandamana.

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita polisi jijini Kinshasa ilisambaratisha maandamano ya wafuasi wa chama cha rais Tshisekedi, cha UDPS baada ya kujaribu kuandamana kupinga uteuzi wa Ronsard Malonda kama mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, CENI.

Hatua ya Bunge la taifa nchini DRC kumteua Ronsard Malonda kuwa mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi (CENI) inaendelea kuzua mvutano nchini DRC.

Chama cha UDPS kinashtumu mshirika wake madarakani FCC kusababisha hali hiyo, kwa kujivunia wingi wa viti katika Bunge.

Kufuatia uteuzi huu mungano madarakanii (CASH na FCC) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umegawanika. Chama cha UDPS kimefutilia mbali uteuzi wa Ronsard Malond kama mwenyekiti wa CENI, kikisema kuwa "utaratibu uliotumiwa na FCC kumteua mgombea wake katika nafasi ya asasi za kiraia ni wa aibu".

Kwa upande wa chama hicho cha rais, mshirika wake madarakani hutumia "mabavu" kwa kutaka kuvunja sheria kwa mambo ambayo yanahitaji makubaliano ya kitaifa.