COTE D'IVOIRE-SIASA

Makamu wa rais wa Côte d'Ivoire Daniel Kablan Duncan ajiuzulu

Daniel Kablan Duncan (hapa ilikuwa Novemba 21, 2012 huko Abidjan).
Daniel Kablan Duncan (hapa ilikuwa Novemba 21, 2012 huko Abidjan). AFP PHOTO / ISSOUF SANOGO

Makamu wa Rais wa Côte d'Ivoire, Daniel Kablan Duncan, amejiuzulu, hatua ambayo imepokelewa na Rais Alassane Ouattara, ofisi ya rais wa Côte d'Ivoire imetangaza.

Matangazo ya kibiashara

Makamu wa rais Côte d'Ivoire, Daniel Kablan Duncan, 77, amejiuzulu wadhifa wake, katibu mkuu wa ofisi ya rais Patrick Achi ametangaza leo Jumatatu, wakati nchi hiyo inaomboleza baada ya kifo cha Waziri Mkuu Amadou Gon Coulibaly aliyefariki dunia Julai 8.

"Makamu wa Rais Daniel Kablan Duncan amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais wa Jamhuri [...] kwa sababu zake kibinafsi Februari 27 [...] baada ya mazungumzo kadhaa, ambayo ya mwisho yalifanyika mnamo Julai 7, hatimaye Rais Alassane Ouattara alikubali na kutia saini sheria inayositisha majukumu ya Bw. Kablan Duncan Julai 8, " imesema taarifa iliyosomwa na Patrick Achi.

"Rais wa Jamhuri amependa kupongeza juhudi alizofanya kigogo huyo, mtu wa busara na ambaye alijitoleakwa kulitumikia taifa", kulingana na taarifa hiyio.

Daniel Kablan Duncan hapo awali alikuwa Waziri wa Mambo ya nje, kisha Waziri Mkuu, kabla ya kuwa Makamu wa Rais. Alikuwa kada wa chama cha PDCI na kisha alifutwa uanachama kwa muda mfupi mnamo mwaka wa 2019 kwa utovu wa nidhamu na kuingilia masuala yasiyomhusu wakati wa mvutano kati ya vyama vya PDCI na RHDP.